1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fedha za kuwahudumia watoto

Hamidou, Oumilkher12 Februari 2008

Mivutano kati ya washirika wa serikali kuu inapaliliwa na kampeni za uchaguzi

https://p.dw.com/p/D6Jd
Kampeni ya uchaguzi HambourgPicha: AP


Mada kuu magazetini hii leo ni pamoja na fedha wanazolipwa wazee kwaajili ya kuwahudumia watoto wao,kima cha chini cha mishahara na hotuba ya waziri mkuu wa Uturuki Tayyep Erdogan mjini Cologne.


Tuanze lakini na malipo kwaajili ya watoto.Vyama  ndugu vya Christian Democratic Union-CDU na Christian Social Union-CSU na washirika wao wa Social Democratic- SPD wangependelea kuona kiwango cha fedha wanazolipwa wazee kwaajili ya kuwahudumia watoto wao kinaongezeka kuanzia mwakani.Kutokana na mvutano uliosababishwa na kadhia hiyo gazeti la KÖLNISCHE ZEITUNG linahisi msimamo huo ni kiini macho tuu:

Gazeti linaendelea kuandika:


"Hoja za chama cha CDU kutaka kuwasaidia familia si chochote chengine isipokua mbinu za kisiasa tuu kuwavutia wapiga kura.Uchaguzi unakurubia Hambourg-mkakati unahitajika.Nacho chama cha SPD ambacho hadi wakati huu kimekua kikipinga  ahadi zozote zile za malipo ya fedha kwaajili ya ulezi wa watoto kwa lengo la kujipendekeza,hakijabadilisha msimamo wake kwasababu ya shida walizonazo familia.Hasha,kimefanya hivyo kwasababu ya kishindo kilichosababishwa na CDU.Kwa hivyo na wao pia wanatumia mbinu za kisiasa."



Maoni kama hayo yameelezewa pia na gazeti la LANDESZEITUNG la mjini LÜNEBURG,linaloandika:


Mvutano wa washirika katika serikali kuu ya muungano kuhusu kupandishwa fedha za malipo ya familia kwaajili ya kuwahudumia watoto ,umelengwa kujikingia kura za wananchi tuu na sio kulipatia ufumbuzi tatizo lenyewe.Hofu za kuwaona wafuasi wa chama cha mrengo wa shoto Die Linke maarufu kwa kutetea masilahi ya umma,ndizo zinazowababaisha.


Gazeti la KIELER NACHRICHTEN linaonya:


"Serikali ya muungano wa vyama vikuu inamwaga fedha za umma kana kwamba nakisi ya bajeti ya siku za nyuma ni jinamizi lililokwisha sahauliwa.Sera za maana kuelekea watoto zina sura nyengine kabisa:zinatanguliza mbele mkakati wa kuimarisha bajeti,ili kizazi kijacho kisiachiwe madeni ya walio watangulia."


 Mada nyengine magazetini inahusu kima chini cha mishahara.Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linahisi huu ni mchezo wa karata walioubuni wana Social Democratic tuu kwaajili ya washirika wao wa CDU.Gazeti linaendelea kuandika:


Kila kwa mara  CDU na CSU wanajikuta wanakabiliwa na lawama kutokana na mvutano waliousababisha kwa kupinga kima cha chini cha mishahara.Hali hiyo inatia uchungu zaidi kwasababu maoni yote ya wananchi yanaonyesha kuunga mkono msimamo wa washirika wao.Mwisho wa machungu haujulikani.Kwa wakati wote ule ambao CDU CSU wataendelea kutia na kutoa katika suala la kima cha chini cha mishahara-SPD nao wataendelea na uzi ule ule,ikilazimika hadi uchaguzi mkuu utakapoitishwa.


Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHASU linahisi suala la kima cha chini cha mishahara katika sekta za waajiriwa wa muda mfupi,"limeshaamuliwa"-gazeti linaendelea kuandika:


"Tutashuhudia malumbano ya kisiasa mpaka tutachoka mnamo wiki zijazo.Hatimae maamuzi hayatapatikana kwasababu ya takwimu wala tarakimu.Kitakachoamua mwishoe ni dhamiri za kisiasa tuu.Uamuzi umepitishwa tangu zamani. Katika suala hilo la kima cha chini cha mishahara ,serikali ya muungano wa vyama vikuu imeacha upenu na mwenye kutaka anapita.Wengi miongoni mwa wafuasi wa vyama ndugu vya CDU CSU wanahisi makosa makubwa yamefanyika.Maridhiano yanawezekana tuu ikiwa mmojawapo wa washirika katika serikali ya muungano atajitolea kufanya hivyo.