1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FBI yathibitisha inachunguza uhusiano wa Trump na Urusi

Iddi Ssessanga
21 Machi 2017

Mkurugenzi wa FBI amekiri kwa mara ya kwanza kwamba shirika hilo linachunguza juhudi za Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani. Pia amepuuza madai ya Trump kwamba Obama alinasa mawasiliano katika jengo lake la Trump Tower.

https://p.dw.com/p/2ZbKd
Washington FBI-Chef Comey vor Geheimdienst-Ausschuss des US-Repräsentantenhauses
Picha: Reuters/J. Roberts

Mbele ya kamati ya Bunge, Mkurugenzi wa FBi alichukuwa hatua isiyo ya kawaida na kuthibitisha juu ya uchunguzi unaoendelea. James Comey anasema hatua ya Urusi kudukuwa uchaguzi huo ilikuwa imedharia kumsaidia Donald Trump, na anasemaanataka kubaini iwapo kulikuwepo na ushirikiano kati ya kampeni ya Trump na Warusi. Mkuu huyo wa FBI alikataa kujibu maswali ya kamati ya Intelijensia ya bunge kuhusu nini hasa na nani uchunguzi wake unahusu, akitoa hoja ya haja ya kulinda uchunguzi huo nyeti.

"Nimepewa idhini na wizara ya sheria kuthibitisha, kwamba FBI kama sehemu ya uchunguzi wetu, inachunguza juhudi za serikali ya Urusi kuingilia uchaguzi wa rais wa mwaka 2016, na hiyo inahusu kuchunguza aina ya viunganishi vyovyote, kati ya watu mmoja wanaohusika na kampeni ya Trump, na serikali ya Urusi," alisema Comey mbele ya kamati ya uchunguziya bunge la Congress.

Washington FBI-Chef Comey vor Geheimdienst-Ausschuss des US-Repräsentantenhauses
Mkuu wa FBI James Comey akizungumza mbele ya kamati ya uchunguzi ya bunge huku mkuu wa NSA Mike Rogers akisikiliza.Picha: Getty Images/AFP/N. Kamm

Atupilia mbali madai ya Trump dhidi ya Obama

Katika pigo la pili kwa rais huyo Mrepublican, Comey alikataa madai ya Trump aliyoyatoa kupitia ukurasa wakewa twita maüema mwezi huu, kwamba mtangulizi wake Barack Obama aliamuru kutegwa kwa mawasiliano ya simu katika jengo la Trump Tower, ambako ndiyo kuna makaazi ya tajiri huyo wa majumba.

"Kuhusiana na tweet za rais juu ya madai ya udukuzi wa mawasiliano ulioelekezwa kwake na utawala uliopita, sina taarifa ya kuunga mkono tweet hizo, na tumeangalia kwa umakini ndani ya FBI. Wizara ya sheria imeniomba kuwafamisha kwamba jibu ni sawa kwa wizara ya sheria na vitengo vyake vyote. Wizara haina taarifa zinazounga mkono tweet hizo."

Trump alirejea madai hayo Ijumaa wiki iliopita wakati alipomkaribisha kansela wa Ujerumani Angela Merkel, hiyo ikiwa saa chache tu baada ya ikulu ya White kurudia madai yasio na uthibitisho kwamba shirika la ujasusi la Uingereza GCHQ huenda lilitumiwa na Obama kumchunguza Trump.

Mkurugenzi wa shirika la usalama wa Taifa NSA, Admiral Mike Rogers, ambaye alihudhuria kikao cha kamati ya bunge pamoja na Comey, alisema uhusiano kati ya washirika hao wawili uliharibiwa. "Nadhani hili linamvunja moyo mshirika muhimu," alisema Rogers

Donald Trump US Präsident
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/J. Bourg

Trump ashauriwa kukiri makosa na kuomba radhi

Leon Panetta, waziri wa zamani wa ulinzi na mkurugenzi wa CIA wakati wa utawala wa Obama, alisema katika mahojiano kwamba Trump anapaswa kukiri kwamba alifanya kosa na kumuomba msamaha rais Obama. Katika tweet yake kabla ya kikao hicho cha bunge, Trump aliandika kwamba Wademocrat walipika na kushinikiza stori ya Urusi kama kisingizio cha kuendesha kampeni mbaya.

Chunguzi zisizopungua nne za bunge zinaendelea kuhusu uingiliaji wa Urusi, ambayo mashirika ya ujasusi yalisema mwezi Januari kwamba uliagizwa na rais Vladmir Putin, na ulilenga kusaidia kampeni ya Trump dhidi ya mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton ambaye Putin alikuwa akimchukia. Wademokrat wanasisitiza kuwa udukuzi huo wa Urusi ulichagia kushindwa kwa mgombea wao.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe.

Mhariri: Daniel Gakuba