1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkenya Kemboi apokonywa medali

Jane Nyingi18 Agosti 2016

Bingwa mara mbili wa mbio za Olimpiki kutoka nchini Kenya Ezekiel Kemboi amepokonywa medali yake ya shaba katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji aliyoishinda Rio nchini Brazil

https://p.dw.com/p/1JkZn
Olympia London 2012 3000 Meter Hindernis
Picha: Reuters

Hatua hiyo ni baada ya Ufaransa kukata rufaa baada ya kubainika Kemboi alikanyanga nje ya mstari wakati wa mbio hizo. Uamuzi huo wa kumpokonya Kemboi medali uliafikiwa zaidi ya saa sita baada ya kukamilika mashindano hayo. Hatua hiyo ilitoa nafasi kwa mfaransa Mahiedine Mekhissi aliyemaliza wa nne kupandishwa hadi nafasi ya tatu na kukabidhiwa medali hiyo ya shaba aliyokuwa amepewa Kemboi.

Baada ya kutazamwa video ya mbio hizo ilibainika mwanariadha huyo kwa wakati mmoja baada ya kuruka kiunzi na maji, alikanyaga nje ya mstari.Taarifa ya kutoka shirikisho la kimataifa la riadha IAAF ilisema chini ya sheria za mbio hizo mwanariadha hapaswi kukanyaga nje ya mstari anapofika mzunguko wenye kona.

Mshindi wa mbio hizo za Rio ni Mkenya Conseslus Kipruto ambae aliweka rekodi mpya ya olimpiki kwa kutumia muda wa saa 8:04.28. Mmarekani Evan Jager alimaliza wa pili kwa kutumia muda wa saa 8:04.28.Tayari Kemboi ametangaza kustaafu katika mbio hizo.

Brasilien Olympische Spiele Rio 2016 - 3000 Meter Hindernislauf - Conseslus Kipruto
Mmarekani Evan Jager (kushoto) na Mkenya Conseslus KiprutoPicha: Getty Images/AFP/J. Samad

Taarifa nyingine ni kuwa polisi nchini Brazil wanamzuilia afisa mmoja mkuu wa kamati ya Olimpiki barani Ulaya Patrick Hickey baada ya kuhusishwa na uuzaji tiketi za mashindano ya Rio kinyume na sheria.Raia huyo wa Ireland mwenye umri wa miaka 71 hata amelazimika kujizulu kwa muda ili kutoa nafasi ya kufanyika uchunguzi.Inashukiwa idadi chache ya watu wanaohudhuria michezo hiyo ya Rio imetokana na tiketi kuuzwa bei ghali kwa njia za kimagendo na maafisa wanaoyasimamia mashindano hayo.

Msemaji wa baraza la michezo ya olimpiki nchini Ireland Maek Adams amesema madai yanayomuhusisha Patrick Hickey ni kuhusu tiketi elfu moja miongoni mwa nyingine millioni 6.5 ambazo zilitolewa kwa michezo ya Rio. Polisi bado hawajawahoji maafisa wengine wa baraza hilo ,ambao wamesema wako tayari kutoa ushahidi. Zaidi ya tiketi elfu moja za michezo ya olimpic zimesitishwa, ikiwemo tiketi za ufunguzi na zile za mbio za riadha, na wachunguzi wanasema madai ya udanganyifu yangeweza kutengeneza zaidi ya euro milioni mbili.

Nayo Kamati ya michezo ya Olimpiki nchini Marekani imethibitisha waogeleaji wawili wa taifa hilo wamezuiwa kuondoka nchini Brazil. Hii ni baada ya polisi kutilia shaka habari walizotoa kuhusu kushambuliwa na kuporwa mali yao mjini Rio. Gunnar Bentz na Jack Conger waliondolewa kutoka kwenye ndege iliyokuwa ikielekea Marekani ili kuhojiwa.

Gunnar Bentz Jack Conger verlassen die Polizeistation Rio Flughafen
Waongeleaji wa Marekani Gunnar Bentz( katikati) na Jack Conger (kulia) wakiondoka kituo cha polisi RioPicha: picture-alliance/AP Photo/M.Pimentel

Waogeleaji hao wawili, pamoja na wanamichezo wawili wa kikosi cha Marekani, wanasema waliporwa na watu wenye bunduki wakiwa kwenye teksi mjini Rio siku ya Jumapili.

Wanamichezo wenzao, Ryan Lochte na James Feigen, pia walizuiwa na jaji kuondoka Brazil. Lochte tayari ameondoka nchini humo lakini taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema Feigen amezuiwa kuabiri ndege iliyokuwa inaelekea Marekani.

Na kutamatisha Wajerumani Laura Ludwig na Kira Walkenhorst waliyazamisha matumaini ya wenyeji Brazil baada kusaidia pakubwa ushindi wa kikosi cha kinamama cha mpira wa wavu wa ufukweni katika fainali za mchezo huo.Wajerumani walishinda seti za 21-18 na 21 kwa 14

Mwandishi: Jane Nyingi/rtre,afp.

Mhariri: Iddi Ssessanga