1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eusebio amepewa mazishi ya kishujaa nchini Ureno

4 Julai 2015

Mabaki ya mchezaji nguli wa kandanda Eusebio da Silva Ferreira, aliyefahamika tu kama Eusebio, yamewekwa katika jumba la kitaifa la Ureno mjini Lisbon

https://p.dw.com/p/1FsZk
Mausoleum Eusébio da Silva Ferreira Allee in Lissabon Portugal António Costa
Picha: João Carlos

Jeneza la Eusebio lilitolewa katika makaburi ya Lisbon hadi katika kanisa la kihistoria la karne ya 17 ambako mabaki ya watu mashuhuri katika historia ya Ureno huwekwa. Rais wa Ureno Anibal Cavaco Silva, alihudhuria mazishi hayo

Idhini ya bunge ilihitajika ili kuuhamisha mwili wa mchezaji huyo. Eusebio ndiye mchezaji wa kwanza wa kandanda kupelekwa katika kanisa hilo la kihistoria. Alifariki dunia Januari 2014 akiwa na umri wa miaka 71.

Mwenge wa Michezo ya Olimpiki Rio 2016 wazinduliwa

Muundo wa mwenge wa Olimpiki ambao utaanza safari yake nchini Brazil kabla ya Michezo ya Olimpiki ya 2016 mjini Rio De Janeiro umezinduliwa jana mjini Brasilia, ikiwa ni chini ya siku 400 kabla ya kuanza michezo hiyo. karibu watu 12,000 watachaguliwa kuubeba mwenge huo utakaofikishwa katika zaidi ya miji 300 na vituo vikuu vya majimbo yote 26 ya Brazil, miezi mitatu kabla ya tamasha hilo kuanza.

Polisi wanashughulikia usalama wa mwenge huo, ambao ni sehemu muhimu ya sherehe za Olimpiki. Meya wa Rio de Janeiro Eduardo Paes, amesema mji huo unajivunia kuwa mwenyeji wa tamasha hilo maarufu sana ulimwenguni

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu