1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU kuzishinikiza Poland na Hungary kuhusu hatma ya bajeti

20 Novemba 2020

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamesema wanaongeza juhudi za kuwashawishi wenzao wa Hungary na Poland kuondoa pingamizi la  kuidhinishwa bajeti ya Umoja wa Ulaya na mpango wa uokozi wa uchumi wa kanda hiyo. 

https://p.dw.com/p/3labN
Brüssel EU-Videogipfel | Ursula von der Leyen, Präsidentin der Europäischen Kommission
Picha: Olivier Matthys/AP Photo/picture alliance

Muda mfupi baada ya mkutano wa viongozi wa kanda hiyo uliofanyika kwa njia ya mtandao, kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema wataendelea kutafuta jibu la msuguano uliojitokeza ambao unatishia juhudi za kanda hiyo kukabiliana na janga la virusi vya corona.

Poland na Hungary zikiungwa mkono Slovenia zilitumia kura ya turufu kuzuia bajeti ya dola Trilioni 2.1 ya Umoja wa Ulaya wakipinga masharti yanayotaka nchi wanachama kuzingatia misingi ya utawala wa sheria kabla ya kupata fedha hizo.

Deutschland Berlin | Angela Merkel Pressekonferenz nach EU-Videogipfel
Kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: Michael Sohn/AFP/Getty Images

Bibi Merkel ambaye nchi yake ni mwenyekiti wa zamu wa Baraza la Umoja wa Ulaya amesema mkwamo uliojitokeza ni tatizo kubwa na kwamba ni vigumu kutabiri mbinu za kupatikana ufumbuzi lakini amezitaka nchi wanachama kutoa nafasi ya masikilizano.

"Hii inamaanisha kuwa tumeshindwa kupeleka nyaraka mbele ya Bunge la Ulaya na hakuna kura itakayopigwa wiki inayokuja, na kwamba tunaendelea na mazungumzo na Poland na Hungary kuona kipi tunaweza kufanya kuhakikisha makubaliano yanafikiwa hapa." amesema Merkel.

Ghadhabu kutoka mataifa mengine wanachama 

Ingawa msimamo huo wa Poland na Hungary siyo jambo la kushangaza, kwa sehemu kubwa umeyakasirisha mataifa mengine ya Ulaya yanayosubiri kwa shauku kupata fedha za kusadia kufufua uchumi zao ulioathiriwa na janga la virusi vya corona.

EU ringt um Finanzpaket I M. Morawiecki -und V. Orban
Warizi mkuu wa Poland Viktor Orban (kushoto) na mwenzake wa Poland Mateusz Morawiecki Picha: Czarek Sokolowski/AP/dpa/picture alliance

Maafisa wakuu wa Umoja wa Ulaya ikiwemo rais wa Baraza Kuu Charles Michel wanataka kuhakikisha muda wa mashauriano na nchi hizo mbili unakuwa mfupi na hata kutoa nafasi ya usuluhishi mwingine kuendelea baada ya bajeti kuidhinishwa.

Serikali zinazoegemea siasa za kizalendo za waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban na mwenzake wa Poland Mateusz Morawiecki hazitaki suala la utawala wa sheria na uzingatiaji misingi ya demokrasia kuwa sehemu ya masharti kwa nchi wanachama kupatiwa fedha za bajeti na mpango wa uokozi.

Kwanini Hungary na Poland hawavutiwi na sharti la utawala bora

Hata hivyo wazo la kufangamanisha fedha za Umoja wa ulaya na Utawala wa sheria linaungwa mkono na mataifa mengi wanachama lakini nguvu ya kura ya turufu ambayo ni haki kwa kila taifa mwanachama wa umoja huo imefanya kuwa vigumu kuzizuia Poland na Hungary kuwaziba midomo wanachama wengine.

Suala la kuenzi utawala wa sheria ni nyeti kwa Hungary na Poland. Poland tayari inakabiliwa na uchunguzi wa Umoja wa Ulaya kwa juhudi zake za kupunguza nguvu za muhimili wa mahakama huku Hungary imekalia kuti kavu kwa ukiukaji mkubwa wa desturi za demokrasia ikiwemo uhuru wa habari chini ya utawala wa Orban.