1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU Ivory Coast

Thelma Mwadzaya30 Desemba 2010

Umoja wa Ulaya unakusudia kuimarisha vikwazo dhidi ya rais Laurent Gbagbo ili kumshinikiza mpaka aondoke madarakani.

https://p.dw.com/p/zrQE

Duru za  kibalozi zimearifu  kuwa Umoja wa Ulaya  utaongeza vikwazo hivyo mwezi ujao kwa lengo la kumbana  rais Laurent Gbagbo mpaka  aondoke  madarakani.

Pamoja na vikwazo hiyvo ni  kuongeza orodha  ya  watu   wa Gbagbo watakaopigwa marufuku  kuingia  katika nchi  za Umoja  wa Ulaya.  Wawakilishi wa serikali 27 za nchi za Umoja wa Ulaya walifikia uamuzi huo kwenye  mkutano wao uliofanyika  mjini Brussels.

Wawakilishi hao wamesema vikwazo zaidi vitawekwa dhidi   ya Gbagbo na wapambe  wake ikiwa pamoja na kuzuia mali za  Gbagbo anaeng'ang'ania  madaraka  pamoja na  zile za  wafuasi wake

Kuanzia mwezi ujao Umoja  wa Ulaya utaongeza idadi  ya watu watakaokumbwa  na  vikwazo hivyo na kufikia  61  kutoka 19.

Mwakilishi mmoja wa kibalozi ameliambia shirika  la  Reuters kwamba palikuwa na makubaliano katika matumaini ya kuchukua hatua nyingine  kuanzia mwezi  januari  dhidi ya  Gbagbo  na wafuasi wake.

Rais huyo alishindwa na mpinzani wake Alassane  Outtara katika uchaguzi wa  rais uliofanyika nchini Cote d'Ivoire mwezi  uliopita.

Umoja wa Ulaya kwanza uliwekwa vikwazo dhidi ya  Gbagbo na wafuasi  wake mwanzoni  mwa mwezi huu ili  kumshinikiza aondoke.

Katika hatua nyingine wizara  ya mambo ya nje ya Ufaransa imefahamisha kwamba Umoja wa Ulaya utawatambua wajumbe wa kiongozi wa  upinzani Alassane  Outtara  kuwa  wawakilishi halali wa Cote d'Ivoire.

Uchaguzi uliofanyika  tarehe  28 mwezi novemba nchini  Cote d'ivoire ulikuwa na  shahaba  ya kuurejesha umoja nchini humo, baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya  mwaka 2002  hadi 2003. Tume  ya uchaguzi ya  muda ilionyesha kuwa kiongozi  wa  upinzani Alassane  Outtara alishinda kwa zaidi  ya  asilimia 8. Lakini hesabu hizo  zilibadilishwa haraka sana na mahakama  ya  katiba ya  Cote d'ivoire inayoongozwa na mshirika mkubwa wa  Gbagbo.

Na ghasia  zilizofuatia baada ya matokeo kutangazwa zimesababisha vifo  vya  watu   zaidi ya 170 na pana  hatari ya kuzuka tena  vita nchini  Cote d'ivoire   .

Katika  hatua nyingine ya kumshinikiza Laurent  Gbagbo,nchi za Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuwatambua  wale mabalozi tu walioteuliwa na kiongozi wa  upinzani Alassane Outtara.

Hatahivyo licha ya hatua hizo  za Umoja wa Ulaya  Gbagbo  bado hajaonyesha dalili yoyote ya kukunjika, badala  yake ameilaumu Ufaransa kwa kuongoza  kampeni ya kimataifa kwa lengo la kumng'oa madarakani.

Mwandishi/Mtullya  Abdu/RTRE/

Mhariri:Mwadzaya,Thelma