1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan atishia kuwaachilia wakimbizi wa Syria Kuingia Ulaya

John Juma
10 Oktoba 2019

Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan ametishia kuwaachilia mamilioni ya wakimbizi wa Syria walioko nchini mwake kuingia Ulaya, endapo Umoja wa Ulaya utaendelea kuikosoa operesheni ya Uturuki dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi.

https://p.dw.com/p/3R2z7
Türkei Ankara | Recep Tayyip Erdogan bei Pressekonferenz
Picha: picture-alliance/AP Photo/Presidential Press Service

Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan amesema vikosi vyake vimewaua wanamgambo zaidi ya 109 kufuatia operesheni walioanzisha jana dhidi ya kundi la kikurdi nchini Syria. Wakati huohuo Erdogan ametishia kuwafungulia milango wakimbizi wa Syria kuingia Ulaya ikiwa, viongozi wa  Ulaya wataendelea kuikosoa operesheni hiyo.

Kwenye hotuba ambayo ameitoa leo kwa wanachama wa chama chake cha AKP mjini Ankara, rais wa Uturuki Tayyip Erdogan, amesema operesheni hiyo inayojumuisha mashambulizi ya angani na ardhini yanaendelea.

Ametoa uhakikisho kuwa kundi la jihadi linalojiita Dola la Kiislamu IS halitakuwepo tena kaskazini mashariki mwa Syria pale watakapoikamilisha operesheni hiyo dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi.

Erdogan amesema wafungwa wa kundi la IS ambao wanapaswa kuendelea kushikiliwa wataendelea kuwa gerezani na wale ambao wameruhusiwa na nchi zao kurejea watapelekwa katika mataifa yao.

Ameushutumu vikali ukosoaji wa kimataifa ambao umeelekezwa katika  operesheni hiyo iliyoanza jana, huku akitishia kuwaachilia kuingia ulaya mamilioni ya wakimbizi wa Kisyria wanaoishi Uturuki.

Operesheni ambayo inafanywa na Uturuki kaskazini mashariki mwa Syria imekosolewa kwa kiasi kikubwa ulimwenguni.
Operesheni ambayo inafanywa na Uturuki kaskazini mashariki mwa Syria imekosolewa kwa kiasi kikubwa ulimwenguni.Picha: Getty Images/AFP/B. Kilic

"Enyi Umoja wa Ulaya! Jiandaeni. Ikiwa mnajaribu kuifanya operesheni yetu ya sasa kuonekana ni uvamizi , basi ni rahisi. Tutafungua milpaka yetu  na tuwaache wahamiaji milioni 3.6 kuja kwenu”. Amesema Rais Erdogan.

Nchi za magharibi zimeikosoa operesheni hiyo ya Uturuki, huku Umoja wa Ulaya ukiitaka Uturuki kusitisha mashambulizi. Msemaji wa Umoja wa Ulaya Maja Kocijancic amesema leo kuwa mashambulizi ya Uturuki yanaongeza zaidi wimbi la wakimbizi wanaotoka Syria na pia yanahujumu vita dhidi ya kundi la IS.

Kocijancic amesema hakuna suluhisho la kijeshi kwa machafuko ya Syria na kwamba suluhisho pekee endelevu ni la kisiasa.

Umoja huo umeongeza kuwa operesheni hiyo inarudisha nyuma matumaini yoyote ya kumaliza machafuko nchini Syria.

Mawaziri wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kuujadili mzozo huo siku ya Jumatatu mjini Luxembourg kabla ya mkutano wa kilele wa siku mbili wa wakuu wa umoja huo.

Nchini Ufaransa, chanzo cha habari cha kidiplomasia kimeeleza kuwa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ufaransa imemuita balozi wa Uturuki aliyeko Paris kutowa maelezo kuhusu operesheni hiyo.

Watu wanaoyakimbia mashambulizi kaskazini mashariki mwa Syria
Watu wanaoyakimbia mashambulizi kaskazini mashariki mwa SyriaPicha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

Hii leo, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana kuijadili Syria. Na Hapo kesho katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg atakutana na Rais Erdogan pamoja na waziri wa mambo ya nchi za nje Mevlut Cavusoglu mjini Istanbul.

Vikosi vya Kikurdi vya Syrian Democratic Forces SDF, ambavyo Uturuki inaviangalia kama kundi la kigaidi lakini ambavyo vimekuwa vikiisaidia Marekani kupambana na kundi la IS nchini Syria, vinadhibiti maeneo makubwa kaskazini mashariki mwa Syria.

Vikosi vya Uturuki vimekuwa vikizisogelea ngome hizo mashariki ya mto Euphrates katika operesheni yao.

Erdogan amesema wanamgambo 109 wa Kikurdi wameuawa tangu operesheni ilipoanza jana.

Vyanzo. DPAE, RTRE, AFPE