1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ennahda yatangaza kushinda uchaguzi Tunisia

Grace Kabogo
7 Mei 2018

Chama cha Ennahda cha nchini Tunisia kimetangaza ushindikatika uchaguzi huru wa kwanza wa manispaa. Uchaguzi huo unachukuliwa kwa umuhimu mkubwa katika kipindi cha mpito cha demokrasia.

https://p.dw.com/p/2xIH4
Kommunalwahlen in Tunesien
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Dridi

Baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa majira ya saa 12 jioni kwa saa za Tunisia, afisa wa ngazi ya juu wa chama cha Ennahda, Lofti Zitoun alisema kuwa chama chake kimeshinda kwa asilimia tano zaidi kikiwa mbele ya chama  cha upinzani cha Nidaa Tounes.

Vyama vya Ennahda na Nidaa Tounes ni vyama washirika katika serikali ya muungano wa kitaifa na vilikuwa vinatarajiwa kutawala katika uchaguzi huo uliocheleweshwa kwa muda mrefu, ambao utashuhudia maafisa 350 wa manispaa kwa mara ya kwanza tangu baada ya vuguvugu la maandamano ya kupigania demokrasia kwenye nchi za Kiarabu mwaka 2011, yaliouondoa madarakani utawala wa kimabavu uliodumu kwa miongo kadhaa.

Zawadi kubwa Ennahda

Zitoun amesema matokeo hayo ya uchaguzi ni zawadi kubwa kwa Ennahda chama chenye uvumilivu na kinachozingatia demokrasia na kwamba chama hicho kilikuwa kikitaka kuwepo kwa makubaliano.

Aidha, msemaji wa Ennahda, Imed Khemiri amesema chama hicho kitaendelea kuhakikisha panakuwepo na makubaliano na washirika wao. Kauli hiyo ameitoa mbele ya wafuasi wa Ennahda, waliokuwa wamekusanyika nje ya makao makuu ya chama hicho huku wakiimba nyimbo za mapinduzi za mwaka 2011.

Afisa wa chama cha Nidaa Tounes, Borhan Bsais amesema chama chake kiko nyuma ya Ennahda kwa asilimia tatu hadi tano. Amesema ni muhimu kuwa vyama hivyo viwili vimeshinda na muhimu kwa ajili ya usawa wa kisiasa nchini Tunisia.

Kommunalwahlen in Tunesien
Rached Ghannouchi (katikati) kiongozi wa EnnahdaPicha: Reuters/Z. Souissi

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Tunisia, asilimia 33.7 ya wapiga kura ndiyo walijitokeza katika uchaguzi huo. Hata hivyo, tume hiyo iliahirisha uchaguzi kwenye vituo vinane vya kupigia kura kwenye eneo la Mdhila, kutokana na makosa katika karatasi za kupigia kura. Ghasia ziliripotiwa kwenye maeneo kadhaa.

Kasoro zajitokeza

Mjumbe wa tume hiyo, Adel Brinsi amesema kuna kasoro kadhaa zilitokea katika vituo vya kupigia kura, lakini hazikuwa kubwa na hazikuathiri matokeo ya uchaguzi huo au utendaji wao wa kawaida.

Imeelezwa kuwa uchaguzi huo uligubikwa na hali mbaya ya kiuchumi, huku changamoto kubwa ikiwa ni kukidhi matarajio ya bajeti za serikali za mitaa ambako serikali kuu ndiyo inafanya maamuzi kuhusu jinsi na wapi fedha zinapaswa kutumika. Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali nchini Tunisia la Jamaity, Nour Kaabi anazungumzia kuhusu hali ya kiuchumi nchini humo.

''Watunisia hawalipi kodi kwa sababu wanasema hawaoni huduma zozote zinazotolewa kila siku kama vile barabara na umeme. Kama raia anagundua kwamba kodi yake inatumika vizuri na kuona manufaa yake, basi manispaa zitakuwa na mapato ya kutosha,'' alisema Kaabi.

Wafadhili wa nchi za Magharibi wanataka kuyasaidia kifedha mabaraza ya manispaa ili kuanzisha miradi mara moja. Hiyo ni juu ya mkopo wa mabilioni ya Dola kutoka kwa Shirika la Fedha Duniani, IMF pamoja na nchi kadhaa kwa ajili ya kusaidia katika upungufu wa bajeti, uliosababishwa na mzozo wa kisiasa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AFP, Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman