1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Eneo la mashariki mwa Kongo lakabiliwa na ukosefu wa chakula

Kabogo, Grace Patricia13 Novemba 2008

Mapigano yanayoendelea mashariki mwa Kongo yamesababisha eneo hilo linalolima nafaka kwa wingi kugeuka eneo la njaa ambako maelfu ya watu walioyakimbia makaazi yao kwa sasa wanategemea chakula kutoka nje.

https://p.dw.com/p/FtrS
Wananchi wa Goma Mashariki mwa Congo, wakikimbia mapigano yanayoendelea katika eneo hiloPicha: AP

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani(WFP), limesema kiwango cha ukosefu wa lishe bora katika eneo la Rutshuru, ambako mapigano yameendelea kwa wiki kadhaa kati ya majeshi ya serikali na ya waasi yanayoongozwa na Jenerali Laurent Nkunda ni kishindo kikubwa ambacho wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya kibinaadamu wanakabiliana nacho, ili kuweza kufikisha mgawo wa misaada hiyo.


Mapigano mapya yamehatarisha shughuli mbalimbali za kibinaadamu zilizoanza tangu miaka ya 1990. Zaidi ya watu milioni 5 wamekufa tangu vita vianze mwaka 1998, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuliko mapigano mengine yoyote kuwahi kutokea tangu kumalizika kwa vita vya Kwanza vya Dunia na idadi karibu yote iliyosababishwa kutokana na njaa pamoja na magonjwa.


Rutshuru ni eneo kubwa katika jimbo la Kivu Kaskazini lenye mvua za kutosha na ardhi yenye rutuba ambako mahindi, maharage, viazi na vitunguu vinachipua kwa urahisi. Lakini eneo hilo limekuwa likikabiliwa na mapigano kwa miaka mingi sasa.


Imeelezwa kuwa watu wengi hawajavuna mazao yao katika misimu mitatu ya mavuno kutokana na mapigano, hivyo kusababisha mfumo wa masoko kubadilika na watu wamekuwa wakishindwa kupanda mazao ya aina mbalimbali kutokana na mapigano hayo.


Mapigano mapya yaliyoanza wakati mpango wa amani kati ya waasi na wanajeshi wa serikali kuvunjika, yamesababisha watu 250,000 kukosa makaazi, na wengine wapatao milioni 1 kutoka Kivu Kaskazini kuyakimbia makaazi yao ndani ya miaka miwili.


Awali Jenerali Nkunda alisema anapigana kwa ajili ya kuwalinda Watutsi wachache dhidi ya mashambulizi ya Wahutu, lakini hivi karibuni alisema malengo yake ni kumuangusha madarakani Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo, hadi hapo atakapokubali kufanya nae mazungumzo ya ana kwa ana.


Afisa wa WFP, Marcus Prior, alisema Rutshuru imekuwa na idadi kubwa ya watu wasiopata lishe bora ambako watu 60,000 hawana makaazi katika mji huo pekee na ambao wanategemea msaada wa chakula na kwamba lazima wafanye kila jitihada za dharura kwa ajili ya kuwafikia.


Kutokana na sababu za kiusalama zilizosababisha shirika hilo kushindwa kusambaza chakula kwa siku kadhaa, shirika hilo lilifanikiwa kugawa biskuti za kuongeza nguvu mwilini katika eneo linaloshikiliwa na waasi karibu na Rutshuru wiki hii ili kupunguza tatizo la utapiamlo kwa watoto. Lakini wafanyakazi wa mashirika ya misaada wamekuwa wakifanya jitihada za kuwatafuta watu wasio na makaazi kwa ajili ya kuwapatia chakula.


Wakati wa migogoro iliyopita, baadhi ya watu wenye mashamba katika maeneo ya karibu walikuwa wakipeleka vyakula katika masoko, lakini kwa sasa suala hilo liko nje ya uwezo wao kutokana na watu wengi wanaoyakimbia makaazi yao kuchukua vifaa kidogo pamoja nao.


Domitira Mbonigaba N'Bahunde, mmoja kati ya watu 5,000 wanaoishi katika matandiko ya plastiki kwenye eneo la Kiwanja alisema kuna vyakula vya aina mbalimbali kwenye masoko, lakini hawawezi kununua bidhaa hizo kwa sababu hawana pesa. Aliongeza kuwa hawawezi kwenda majumbani kwao na hawana chakula kabisa.