1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Duru ya tatu ya uchaguzi wa bunge imeanza Misri

Wananchi katika majimbo tisa ya Misri wanapiga kura katika duru ya tatu ya uchaguzi wa wabunge. Majimbo hayo ni ngome ya vyama vya Kiislamu, ambavyo vimepata ushindi katika duru za awali.

Wananchi wa Misri wameitikia kwa wingi zoezi la kupia kura

Wananchi wa Misri wameitikia kwa wingi zoezi la kupia kura.

Takribani wapiga kura milioni 14 wanashiriki katika uchaguzi wa leo na kesho katika majimbo tisa kati 27 ya Misri. Makundi ya Kiislamu yanategemewa kujiongezea ushindi baada ya kufanya vyema katika duru mbili za kwanza, na kujihakikishia udhibiti wa bunge lenye viti 498.

Muungano kati ya kikundi kikubwa kabisa cha kiislamu nchini Misri cha Udugu wa Kiislamu, na kikundi kingine cha waislaamu wenye msimamo mkali wa kisalafia cha Al -Nour, ulijikusanyia asilimia 70 ya kura kutoka duru mbili za awali. Waliberali na makundi yasio ya kidini ambao waliongoza harakati za kuung'oa utawala wa Rais Hosni Mubarak wamepata kura chache katika uchaguzi huu ambao ulianza tarehe 28 Novemba 2011.

Wapiga kura wameyapa ushindi mkubwa makundi ya kiislamu

Wapiga kura wameyapa ushindi mkubwa makundi ya kiislamu

Idadi kamili ya viti kwa kila kikundi haiwezi kujulikana sasa kutokana na ugumu wa mfumo wa uchaguzi ambao unafuatwa nchini Misri. Katika mfumo huo, baadhi ya viti hushindaniwa baina ya wagombea binafsi, wakati vingine hugawanywa kwa vyama kulingana na wingi wa kura vilizopata katika zoezi zima la uchaguzi.

Tume ya uchaguzi itatangaza idadi halisi ya viti vya kila kikundi bungeni baada ya kukamilika kwa mchakato mzima ifikapo tarehe 13 mwezi huu. Jukumu la kwanza la bunge litakalochaguliwa litakuwa kuteua baraza la watu 100, ambalo litatayarisha rasimu ya katiba mpya.

Wachunguzi walisifia jinsi zoezi la kupiga kura lilivyoendeshwa katika duru mbili zilizotangulia, lakini hatua ya vyombo vya usalama kuvamia ofisi za mashirika ya kimataifa wiki iliyopita, kulizusha lawama kuwa huenda ilikuwa na dhamira ya kuyazuia mashirika hayo kuendelea kufuatilia uwazi katika uchaguzi huo.

Pia waliberali na makundi yasio ya kidini walivishutumu vikundi vya kiislamu, hususan Udugu wa Kiislamu na chama cha Al-Nour, kutumia kauli-mbiu za kuhadaa umma, ambamo walisema wapinzani wao si wacha mungu. Muhamed Abu Hemed kutoka chama cha Free Egyptians alisema katika duru hii ya uchaguzi wamelazimika kutoa ujumbe kuwahakikishia wapiga kura kwamba wanaheshimu dini.

Fujo zilijitokeza katika maandamano ya wapenda mageuzi

Fujo zilijitokeza katika maandamano ya wapenda mageuzi

Wamisri wana kiu ya kuona hali ya utulivu ikirejea baada ya karibu mwaka mzima wa harakati za kutaka mageuzi. Baraza la kijeshi linalotawala nchi hiyo limekuwa likiwekewa shinikizo kuharakisha utaratibu wa kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia, na katika kuitikia mbinyo huo Jumapili lilitangaza kuwa uchaguzi wa baraza la seneti utakuwa wa duru mbili badala ya tatu

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/RTRE

Mhariri: Othman, Miraji