1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yazidi kuisaka amani ya Syria

16 Mei 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, anakutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi na Rais Barack Obama wa Marekani anafanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan, juu ya Syria.

https://p.dw.com/p/18ZRc
South Korean Foreign Minister Ban Ki-moon talks to the reporters during his press conference at the Foreign Correspondent Club in Seoul Thursday, Oct. 20, 2005. Ban said North Korea must provide the details of its nuclear weapons program and facilities if a recent agreement for the communist state to abandon them is to be implemented.(AP Photo/Ahn Young-joon)
Ban Ki MoonPicha: picture-alliance/AP

Ikulu ya Urusi, Kremlin, imesema kwamba Rais Putin amepangiwa kukutana na Ban Ki-moon katika makaazi yake yaliyoko mji wa Sochi siku ya Ijumaa.

Licha ya Kremlin kutotaja ajenda ya mazungumzo ya viongozi hao wawili, lakini ziara ya siku tatu ya Ban Ki-moon nchini Urusi inayoanza leo, inafanyika katika wakati ambapo kuna shinikizo la kimataifa la kufanyika kwa kongamano litakalomaliza miaka miwili ya mauaji nchini Syria.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Urusi na Marekani zilipendekeza kuitisha mkutano wa amani juu ya Syria, unaotarajiwa kutuwama juu ya makubaliano yaliyofikiwa mwezi Juni jijini Geneva na ambayo kamwe hayajawahi kutekelezwa.

Makubaliano hayo yalitaka kusitishwa kwa mapigano na kuundwa kwa serikali ya mpito. Mkutano uliopendekezwa na Urusi na Marekani pia utafanyika Geneva mwezi ujao.

Hata hivyo, Urusi haioneshi dalili yoyote ya kuacha kuunga mkono utawala wa Rais Bashar al-Assad, na imekataa waziwazi kutumwa kwa silaha za kujilinda kwa wapinzani wa utawala huo.

Azimio la Umoja wa Mataifa

Hapo jana, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilimlaani Assad kwa kuendeleza vita vya Syria, lakini kwa mara nyengine Urusi ililipinga azimio hilo lililopitishwa kwa kura 107 dhidi ya 12 kwenye Baraza hilo lenye wajumbe wajumbe 193.

Balozi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa, Bashar Ja'afari, akizungumza dhidi ya azimio la Umoja huo.
Balozi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa, Bashar Ja'afari, akizungumza dhidi ya azimio la Umoja huo.Picha: Getty Images

Iran imeliita azimio hilo la jana kuwa ni la kuyapa nguvu makundi ya kihalifu na ya siasa kali kuendeleza vitendo vya mauaji. Msemaji wa mambo ya nje wa Iran, Abbas Araqchi, amehoji muda ambao azimio hilo limetolewa, akisema kwamba limekuja kuzuia juhudi za kimataifa kutafuta suluhisho kwa njia za amani.

Iran, ambayo kama ilivyo Urusi ni muungaji mkono mkubwa wa utawala wa Assad, inayachukulia makundi yote ya upinzani nchini Syria kuwa magaidi wanaopewa msaada na mataifa ya Magharibi.

Kura ya jana ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na ziara ya Ban Ki-moon nchini Urusi, zinasadifiana na mkutano wa Rais Obama wa Marekani na Waziri Mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan, jijini Washington hivi leo.

Uturuki yaja juu

Uturuki, ambayo ni mwanachama wa Shirika la Kujihami la NATO, ni muhusika mkuu kwenye mgogoro wa Syria kutokana na nchi hizo mbili kuchangiana mpaka. Kiasi cha wakimbizi 400,000 wa Syria wako nchini Uturuki, na mara kadhaa serikali mjini Ankara imekuwa ikitoa kauli kali dhidi ya utawala wa Assad.

Jamaa za watu waliouawa kwenye mashambulizi ya mabomu kwenye mji wa Reyhanli, mpakani mwa Uturuki na Syria.
Jamaa za watu waliouawa kwenye mashambulizi ya mabomu kwenye mji wa Reyhanli, mpakani mwa Uturuki na Syria.Picha: Reuters

Rais wa Uturuki, Abdullah Gul, hivi leo amekosoa namna jumuiya inavyoushughulikia mgogoro wa Syria, ambao hadi sasa umeshagharimu maisha ya zaidi ya watu 90,000.

Akizungumza katika mji wa Reyhanli ambako bomu lililotegwa kwenye gari liliwaua watu 51 mwishoni mwa wiki, Rais Gul amesema ulimwengu unatumia lugha ya mafumbo badala ya kulitatua tatizo.

"Mchango wa jumuiya ya kimataifa kwa msaada wa kifedha wa Uturuki kwa watu hawa walio kwenye hali ngumu ni maneno tu. Kutoka awali, dunia imekuwa ikitumia kauli za balagha na vijembe tu katika mgogoro wa Syria", amesema Rais Gul.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman