1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaadhimisha miaka 70 ya kumalizika Vita vya Pili

Mohammed Khelef8 Mei 2015

Dunia inaadhimisha miaka 70 ya kumalizika kwa Vita vya Pili ya Dunia kufuatia kujisalimisha bila masharti kwa jeshi la Kinazi la Ujerumani mbele ya jeshi la Muungano wa Jamhuri za Kisovieti tarehe 8 Mei.

https://p.dw.com/p/1FMjS
Viongozi wa dunia kwenye maadhimisho ya 70 ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia.
Viongozi wa dunia kwenye maadhimisho ya 70 ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia.Picha: picture-alliance/epa/A. Warzawa

Tukio hili linaloadhimishwa barani Ulaya kwa jina la "Siku ya Kumbukumbu na Maridhiano" linafanyika, huku mzozo wa hivi karibuni kati ya Urusi na mataifa ya Magharibi unaotokana na tuhuma za magharibi juu ya ushiriki wa Urusi kwenye siasa za Ukraine, ukiwa umeyafanya mataifa kadhaa ya Magharibi kuususia mchango huo muhimu wa Urusi kwenye historia yao.

Mjini Berlin, bunge la Ujerumani liliiadhimisha siku hii ambayo miaka 70 iliyopita jeshi lake lilijisalimisha bila masharti na bunge lilitambua kwa mara nyengine dhima ya utawala wa wakati huo kwa uharibifu ulioisababishia Ulaya nzima.

"Tarehe 8 Mei ilikuwa siku ya ukombozi kwa bara zima la Ulaya kwa ujumla wake. Tunaomboleza hivi leo kwa mamilioni ya wahanga wa kampeni mbaya kabisa ya kuyaangamiza mataifa na watu wengine, dhidi ya Waslav na dhidi ya Mayahudi wa Ulaya," Spika Norbert Lammert aliliambia bunge hilo.

Spika huyo alifika umbali wa hadi kuwalaumu watu wa Ujerumani kwa kumuunga mkono dikteta Adolf Hitler hadi mwishoni kabisa, akiongeza kwamba siku ya leo si siku ya ukombozi binafsi wa Ujerumani, ingawa amekumbusha kuwa majaribio machache yaliyofanywa na baadhi ya Wajerumani kumuua Hitler hapo kabla yanastahiki kupongezwa na kutukuzwa. Kumbukumbu hizo za leo asubuhi zilihudhuriwa pia na Kansela Angela Merkel na maafisa kadhaa wa ngazi za juu serikalini.

Poland yakumbuka Vita vya Pili

Sherehe kama hizo zilifanyika pia nchini Poland usiku wa manane hapo jana kwenye mji wa Gdansk, ambako zilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, Rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk ambaye mwenyewe ni Mpoland, na marais wa Ukraine na nchi nyengine kadhaa za Ulaya ya Mashariki. Mji huo ndio mahala pa kwanza kushuhudia na kuumia kwenye vita hivyo chini ya mikono ya jeshi la Kinazi mwaka 1939.

Maadhimisho ya miaka 70 ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia nchini Ukraine.
Maadhimisho ya miaka 70 ya kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia nchini Ukraine.Picha: Reuters/V. Ogirenko

Siku ya Jumamosi kutafanyika kile kinachoitwa Gwaride la Ushindi kwenye mji mkuu wa Urusi, Moscow, ambako takribani viongozi 20 wa kilimwengu watahudhuria, akiwemo Ban Ki-moon, Rais Xi Jinping wa China na Raul Castro wa Cuba.

Hata hivyo, hakuna nchi hata moja ya Magharibi iliyokubali kuhudhuria sherehe hizo, kwa sababu ya tafauti za kisiasa kati ya Urusi na mataifa hayo juu ya mzozo unaoendelea sasa nchini Ukraine.

Vita vya Pili vya Dunia vilianza pale wanajeshi wa Kijerumani walipoingia Poland mwezi Septemba 1939 na vilimalizika pale mkuu wa majeshi wa Ujerumani, Wilhelm Keitel, aliposaini waraka wa kujisalimisha usiku wa manane wa siku kama ya leo kwenye makao makuu ya jeshi la Kisovieti mjini Berlin.

Ingawa kusalimu huko amri kwa jeshi la Kinazi kulivimaliza Vita hivyo barani Ulaya, mgogoro huo uliendelea barani Asia hadi mwezi Agosti 1945, ukikisiwa kuangamiza maisha ya watu milioni 60 duniani kote.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf