1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC yaridhishwa kuondoka kwa M23 Goma

3 Desemba 2012

Siku mbili baada ya waasi wa M23 kuondoka mjini Goma, maisha yameanza kuwa ya kawaida japo si kama hapo mwanzoni, wakati mjini Kinshasa serikali ikiifungia Radio Okapi kwa kuwapa nafasi waasi hao kwenye matangazo yake.

https://p.dw.com/p/16ufF
Waasi wa M23 wakiondoka Goma.
Waasi wa M23 wakiondoka Goma.Picha: AP

Shughuli za kawaida zimeanza kurejea katika mji wa mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Goma, lakini sio kama ilivyokuwa hapo mwanzoni. Bado benki kadhaa hazijafungua huduma zake na hata baadhi ya shule zilizokuwa zimekwishafunguliwa, zimewarudisha watoto majumbani kwao bila kutoa sababu maalum.

Kwa upande mwengine, viongozi wa serikali kuu kutoka Kinshasa wameanza kuutembelea mji wa Goma kutathmini hali ilivyo, mmoja wao akiwa Kamishna Mkuu wa Polisi. Serikali ya Kongo imefurahishwa na kuondoka kwa waasi wa M23 mjini Goma na vitongoji vyake.

Serikali yaridhishwa na kuondoka kwa M23

Msemaji wa serikali ya Kongo, Lambert Mende, ameelezea hatua hiyo kuwa ni mwanzo wa taratibu ya kurejesha amani na usalama kwenye jimbo la kivu ya kaskazini.

Waasi wa M23 wakiondoka Goma.
Waasi wa M23 wakiondoka Goma.Picha: AP

Mende ameiambia DW kwamba kuondoka kwa waasi wa M23 ni moja ya hatua katika juhudi za kutafuta amani.

"Serikali imepokea vyema kuondoka kwa waasi wa M23 kwenye mji wa Goma na vitongoji vyake, ikiwa ni hatua moja wapo ya taratibu ya kurejesha utulivu. Siku za baadaye Raïs Kabila atatafakari kuhusu madai ya waasi kutokana na mkataba wa Machi 2009."

Mende amesema pia kwamba uchunguzi upya wa malalamiko ya waasi hakumaanishi kwamba ni mwanzo wa mazungumzo mapya baina ya serikali na waasi hao wa M23.

Akijibu kuhusu matamshi ya kiongozi wa kijeshi wa kundi la M23 ambaye aliahidi kurejea tena Goma ikiwa mazungumzo hayatofanikiwa, Mende amesema kwamba hakuna mtu yeyote atakayewaruhusu tena waasi hao kuuteka mji huo.

"Hivyo ni vita vya kisaikolojia anavyovieleza Makenga, lakini ukweli ni kwamba historia haiandikwi kabla. Hakuna mtu yeyote atakayewaruhusu waasi hao kurejea tena Goma."

Serikali imetangaza kuwapeleka polisi 500 mjini Goma ambao watahusika na usalama wa mji huo, huku kikosi cha wanajeshi wa Kongo na kile cha kimataifa kikitarajiwa kuwasili katikati mwa wiki hii.

Umoja wa Mataifa waitaja tena Rwanda

Huku juhudi za kutafuta amanai zikiendelea kwenye kanda ya Maziwa Makuu, ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inaelezea kwamba wanajeshi wa Rwanda walikuwa kwenye mstari wa mbele katika kuuteka mji wa Goma.

Kiongozi wa tawi la kisiasa la M23, Jean-Marie Runiga.
Kiongozi wa tawi la kisiasa la M23, Jean-Marie Runiga.Picha: Reuters

Ripoti hiyo iliotolewa kwenye gazeti la New York Times la Marekani inaelezea kwamba mashambulizi ya Goma yalipangwa mjini Kigali, Rwanda. Ripoti hiyo mpya inaeleza kwamba Jenerali Bosco Ntaganda aliongoza vita vya Kibumba. Wanajeshi wa Rwanda wapatao 1,000 walivuuka mpaka na kuunga mkono waasi wa M23 kwa kuuteka mji wa Goma, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Ripoti hiyo inaelezea kwamba waasi wa M23 walipewa sare mpya ya kijeshi ambazo inatafautiana kidogo tu na zile za jeshi la Rwanda. Serikali ya Kongo haijatoa taarifa yoyote kufuatia madai hayo mapya.

Redio ya Umoja wa Mataifa yafungiwa

Wakati huo huo, Hamlashauri Kuu ya Habari (CSAC) imepiga marufuku matangazo ya Radio Okapi inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa kwa siku nne. Viongozi wa Redio Okapi wamesema kwamba amri hiyo inatokana na wao kuwapa nafasi ya kujieleza viongozi wa waasi wa M23, lakini mkuu CSAC, Jean Bosco Bahala, amesema kwamba hatua hiyo inatokana na Redio Okapi kwenda kinyume na mipangilio ya matangazo yake.

Waasi wa M23 wakiondoka Goma.
Waasi wa M23 wakiondoka Goma.Picha: AP

Halmashauri ya CSAC imeitahadharisha Radio France Internationale (RFI) juu ya mfumo wake wa matangazo yanayoihusu DRC ambayo inaelezewa kuwa yanatishia usalama wa kitaifa na yanachochea ukabila.

Ripoti: John Kanyunyu, Goma/Saleh Mwanamilongo, Kinshasa
Mhariri: Mohammed Khelef