1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC yaanzisha mashambulizi dhidi ya FDLR

25 Februari 2015

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo limeanzisha mashambulizi dhidi ya waasi wa kundi la Kihutu kutoka Rwanda-FDLR, walioko mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1EgwH
Wanajeshi wa serikali ya Kongo-FARDC
Wanajeshi wa serikali ya Kongo-FARDCPicha: Getty Images/AFP/Alain Wandimoyi

Operesheni hiyo dhidi ya FDLR iliyoanza jana katika jimbo la Kivu ya Kusini, itadumu hadi waasi hao watakaposabaratishwa kabisa. Kiongozi wa mji wa Lemera, Innocent Ndaheba, amesema milio ya silaha nzito nzito pamoja na miripuko ilisikika kwenye eneo la Lemera lililoko umbali wa kilomita 30 kutoka Mulenge. Amesema vikosi vya jeshi la serikali ya Kongo, FARDC, vilianza kupelekwa katika eneo hilo siku mbili zilizopita.

Afisa mmoja wa jeshi la Kongo ambaye hakutaka kutajwa jina lake ameliambia shirika la habari la AFP kwamba jeshi limechukua hatua madhubuti kuhakikisha linawalinda raia. Hata hivyo, mkaazi mmoja wa Mulenge, Gode Mutama ambaye anaishi kilomita chache na zinapoendelea operesheni hizo, amesema wana hofu kuwa operesheni hizo zitasababisha madhara makubwa.

Afisa huyo wa jeshi amethibitisha kuwa operesheni hizo zinafanyika chini ya kamanda wa jeshi, Brigedia Jenerali Espera Masudi katika mkoa wa Mulenge, Uvira. Mwezi uliopita Rais Joseph Kabila wa Kongo, alitangaza kuwa operesheni hiyo itaungwa mkono na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo-MONUSCO, ambapo kitatoa msaada wa vifaa na operesheni.

Rais Joseph Kabila
Rais Joseph KabilaPicha: AFP/Getty Images/A. Wandimoyi

Hata hivyo, MONUSCO ilijiondoa katika operesheni hiyo ya pamoja baada ya Kongo kukataa kuwaondoa majenerali wawili wa jeshi Bruno Mandevu na Fall Sikabwe, ambao wanatuhumiwa na Umoja wa Mataifa kwa kukiuka haki za binaadamu. Majenerali hao walikuwa wameteuliwa kuongoza operesheni hizo.

Marekani yaitaka DRC kumaliza vitisho vya FDLR

Wakati huo huo, Marekani imeitaka Kongo kumaliza vitisho vinavyoweka na waasi wa FDLR wanaojificha katika majimbo ya mashariki mwa Kongo. Mjumbe maalum wa Marekani katika ukanda wa Mazima Makuu anayemaliza muda wake, Russ Feingold, ameutoa wito huo jana wakati wa kuzinduliwa kwa operesheni za kijeshi dhidi ya waasi hao, zilizokuwa zikisubiriwa kwa muda mrefu.

Wapiganaji wa FDLR
Wapiganaji wa FDLRPicha: DW/S. Schlindwein

Mjumbe huyo wa Marekani amesema hatua la kuangamizwa kwa waasi wa FDLR, ni jukumu la kimataifa. Amesema hakuna kundi lolote lile lenye silaha na hasa ambalo liko kwenye orodha ya waliofanya mauaji na ukatili likiwemo kundi la FDLR, ambalo linapaswa kusalimika.

Waasi wa FDLR wamekuwa wakiendesha shughuli zake katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu ya Kusini, tangu walipovuka mpaka kutoka Rwanda mwaka 1994 na kuingia katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Waasi hao wanashutuhumiwa kuhusika na mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994, ambapo watu 800,800 waliuawa wengi wao wakiwa Watutsi.

Kundi la FDLR linalokisiwa kuwa na wapiganaji 1,500 hadi 2,000, lilikaidi amri ya Jumuiya ya Kimataifa ya kusalimisha silaha Januari Pili mwaka huu, tarehe ambayo ilikuwa imewekwa rasmi kwa ajili ya kuweka chini silaha hizo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman