1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Diplomasia ya China nchini Sudan

P.Martin22 Septemba 2007

Wanajeshi wa China watakapoungana na kikosi cha amani cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan katika mwezi wa Oktoba,majeshi hayo yataashiria uhakika mpya wa kidiplomasia wa serikali ya Beijing. Wakati huo huo,watadhihirisha msimamo mpya wa China ambayo hapo awali ilikuwa ikikataa kabisa kuingilia mambo ya ndani ya nchi zingine.

https://p.dw.com/p/CH7t
Wakimbizi wa Darfur wakipiga foleni kupata maji katika kambi ya Abu Shouk
Wakimbizi wa Darfur wakipiga foleni kupata maji katika kambi ya Abu ShoukPicha: AP

China kwa kupeleka wanajeshi wake wa amani Darfur,inasafirisha pia aina mpya ya udiplomasia ikitumai kuwa utasaidia maslahi yake kama dola linalozidi kuwa na usemi.Kwani China iliyofumuka kiuchumi bila ya kufuata mfumo wa kidemokrasia wa magharibi,hupendelea kutoa misaada ya uchumi na maendeleo isiyofungamanisha mageuzi ya kisiasa.

Msimamo huo wa China unadhihirika waziwazi nchini Sudan,ambako Beijing hutazamwa kama dola lenye usemi mkubwa.Sababu ni kwamba China hununua theluthi mbili ya mafuta yanayotoka Sudan na serikali ya Khartoum inapatiwa silaha.

China inapinga mito ya jumuiya ya kimataifa kuiwekea vikwazo serikali ya Sudan inayotuhumiwa kuunga mkono matumizi ya nguvu katika jimbo la magharibi la Darfur.Kama mwanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,China imetumia kura turufu kuzuia juhudi za nchi za magharibi kuiwekea vikwazo Sudan.Vile vile ilishikilia,vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa vipelekwe Darfur kwa idhini ya Khartoum.

Maafisa wa Kichina wanaendelea kupinga lawama za kimataifa kuwa msaada wa Beijing kwa serikali ya Sudan,unachangia kurefusha maafa ya binadamu katika jimbo la mgogoro la Darfur.Vile vile,China inashikilia kuwa ukuaji imara wa kiuchumi utaleta hali bora ya maisha na kuongeza mapato na hivyo migogoro ya kijamii itapunguka.Kwa maoni yake, msaada wa kiuchumi utakaotokomeza umasikini,ni njia bora zaidi ya kuisaidia Sudan na si vikwazo.

Wakati huo huo wataalamu wa Kichina wanasema, baada ya kufanywa majadiliano ya miezi na miezi,Khartoum imeruhusu kupeleka Darfur kikosi cha amani cha wanajeshi 26,000 wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa,kufuatia juhudi za kidiplomasia za Beijing na msimamo wake imara wa kuiunga mkono serikali halali ya Khartoum.

Hata wakosoaji wakali wa China wanakubali kuwa Beijing imetoa mchango mkubwa katika uamuzi wa serikali ya Sudan na vile vile kuishawishi kuhudhuria mkutano pamoja na makundi ya waasi nchini Libya katika mwezi wa Oktoba.

Lakini,baadhi ya wakosoaji wanabisha kuwa China kwa ghafula,imechangamka kuchukua hatua kwa sababu ya kampeni ya kimataifa inayofungamanisha mauaji ya Darfur na Michezo ya Olimpiks ya mwaka 2008 mjini Beijing.Kwani wanaharakati wanaogombea haki za binadamu pamoja na waigizaji maarufu wa michezo ya sinema,wameungana kutoa mito ya kususia michezo ya Beijing,ikiwa China haitojitahidi zaidi kuzuia mapigano katika jimbo la Darfur.

Zaidi ya watu 200,000 wameuawa na wengine wapatao milioni 2.5 wamepoteza makazi yao,tangu mapigano ya Darfur kuanza katika mwaka 2003.