1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Deutsche Welle mambo yote

23 Januari 2013

Bismi mwanzo shairi, nami nangia mwanjani Kueleza kwa uzuri, nilonayo mawazoni Yahusuyo mahodari, Redio Ujerumani Deutsche Welle mambo yote, hongera za kuzaliwa.

https://p.dw.com/p/17QI9
DW Kisuaheli Team aus den 90-iger Jahren in Köln.
50 Jahre Kisuaheli RedaktionPicha: DW

Utitiri wa redio, waibuka duniani
Wazidi kila uchao, unazongana hewani
Deustche Welle baba lao, yakamata usukani

Kwa habari za hakika, za kweli iliyo wazi
Tena za kuaminika, zisizo na uchochezi
Deustche Welle umefika, si ‘watu wa gozi gozi’

Watangazaji fasaha, sauti za kuvutia
Hutangaza kwa madaha, tena bila kukosea
Kuwasikiliza raha, furahani hukutia

Vipindi vyao ni bora, vyote ni vyenye kufaa
Mbele ya Meza Duara, Jukwaa la Manufaa
Na Mtu na Mazingira,   Tamaduni na Sanaa

Afrika Wiki hii, nayo Mbiu ya Mnyonge
Kama si redio hii, tungeachwa na mawenge
Tungewa hatusikii, ingebidi tusiringe

Yangu mimi Deustche Welle, redio niipendayo
Hata na wangu wavyele, wanasikiza iyo iyo
Viremwe na wanakele, huwambii kitu kwayo

Nia yangu sibadili, kukupenda Deustch Welle
Nitakwenda nawe mbali, tena kila kipengele
‘Takushika kweli kweli, sitakuacha milele
Deutsche Welle mambo yote, hongera za kuzaliwa.

Tanbihi:Shairi hili limetumwa na Makame Khamis Mohamed wa Zanzibar kwa ajili ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle.

Mhariri: Mohammed Khelef