1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DAKAR : Wahamiaji wa Kiafrika waokolewa baharini

27 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC6k

Takriban wahamiaji 100 wa Kiafrika ambao mashua yao imepinduka katika bahari ya Atlantiki wakati wakijaribu kufika kwenye visiwa vya Canary wamewasili nchini Senegal baada ya kuokolewa.

Waafrika 89 wengi wao wakiwa ni raia wa Senegal wamenusurika na mkasa huo na wameokolewa nje ya mwambao wa Mauritania na meli ya uvuvi ya Uhispania na baadae kuchukuliwa na meli nyengine ya Uhispania yenye vifaa vya matibabu.Watu wawili wamekufa kutokana na kushuka kwa hali ya ujoto mwilini kunakosababishwa na kupigwa na baridi kwa muda mrefu na wale walionusurika wanasema wamezirusha baharini maiti nyengine za watu 10.

Katika jaribio la kuukimbia umaskini na kutafuta maisha bora barani Ulaya maelfu ya Waafrika huwa wanajaribu kila mwaka kufika kwenye visiwa vya Canary vya Uhispania.

Hapo mwaka 2006 pekee zaidi ya wahamiaji wasio halali 30,000 walifanikiwa kuingia kwenye visiwa hivyo vya Canary.