1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cyprus yasalimika dakika za mwisho

25 Machi 2013

Cyprus iliepuka kutangazwa muflisi baada ya kufikia makubaliano ya dakika za mwisho na wakopeshaji wa kimataifa, katika mazungumzo magumu yaliyodumu kwa masaa 10.

https://p.dw.com/p/183YO
Rais wa Cyprus Nicos Anastasiades.
Rais wa Cyprus Nicos Anastasiades.Picha: Reuters

Makubaliano juu ya mpango mpya wa uokozi wa nchi hiyo yalifikiwa usiku wa manane na kutangazwa saa chache tu kabla ya muda wa mwisho uliyowekwa kuzuia kuanguka kwa mfumo wa benki, kufuatia mazungumzo makali kati ya Rais Nicos Anastaciades na viongozi wa Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Ulaya na shirika la fedha la kimataifa IMF.

Mkuu wa IMF Christine Lagarde, waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfang Schäuble, na waziri wa uchumi na fedha na biashara ya nje wa Ufaransa, Pieree Moscovici.
Mkuu wa IMF Christine Lagarde, waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfang Schäuble, na waziri wa uchumi na fedha na biashara ya nje wa Ufaransa, Pieree Moscovici.Picha: AFP/Getty Images

Mageuzi katika mabenki

Chini ya makubaliano ya mpango huo ambao uliidhinishwa mara moja na mawaziri wa fedha wa kanda inayotumia sarafu ya euro, benki mbili kubwa zaidi nchini Cyprus zitafanyiwa mageuzi, ambapo Benki ya Cyprus iliyo na theluthi moja ya amana zote na inayochukuliwa kuwa benki nzuri itaendelea kufanya kazi, huku benki ya Laiki ambayo ndiyo ya pili kwa ukubwa na yenye matatizo makubwa zaidi ikifungwa, na fedha za wateja wadogo kuhamishwa katika benki ya Cyprus.

Mpango wa sasa ni tofauti na ule wa awali ambao ulipendekeza kutozwa kodi kwa amana zote za wateja wakubwa na wadogo. Mwenyekiti wa kundi la mawaziri wa kanda inayotumia sarafu ya euro, Jeroen Dijsselbloem alisema chini ya mpango huu mpya kodi kwa amana zilizomo katika sekta mzima ya benki inaweza kuepukwa na kwa hivyo itaepukwa. "Kwa ujumla kutakuwa na kupunguza kwa ukubwa wa sekta ya kifedha nchini Cyprus ili ifikie wastani wa Umoja wa Ulaya kufikia mwaka 2018, na napenda kusisitiza kuwa hakuna kati ya hatua hizi itakayoathiri amana za chini ya euro laki moja," alisema Dijsselbloem ambaye pia ni waziri wa fedha wa Uholanzi .

Lakini wateja walio na zaidi ya euro 100,000 wanakabiliwa na kodi ya mara moja, ambayo baadhi ya taarifa zinasema inaweza kufikia hadi asilimia 40. Hii itapelekea kupatiwa fedha za uokozi kiasi cha euro bilioni kumi kutoka benki kuu ya Ulaya na shirika la fedha la kimataifa IMF, ambazo kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa mfuko wa uokozi wa Umoja wa Ulaya Klaus Regling, zitaanza kutolewa mapema mwezi Mei.

Mamia ya wafanyakazi benki wakiandamana nje ya wizara ya fedha mjini Nicosia.
Mamia ya wafanyakazi benki wakiandamana nje ya wizara ya fedha mjini Nicosia.Picha: Reuters

Rais Anastasiades atishia kujiuzulu

Rais Nicos Anastaciades alisema baada ya mfululizo wa mikutano ya majadiliano kuwa makubaliano yaliyofikiwa yalikuwa katika maslahi ya raia wa Cyprus, huku waziri wake wa fedha Michael Sarris akisema anaamini wamepata matokeo bora zaidi yanayowezekana katika hali iliyokuwepo. Jitihada za awali kufikia makubaliano zilishindwa wiki iliyopita baada ya bunge la Cyprus kuukataa mpango uliopendekeza kukatwa kodi kwa amana zote za benki.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wonfgang Schäuble alisema bunge la Cyprus halitahitaji kuupigia kura mpango huu mpya, kwa kuwa tayari waliunda sheria inayobainisha utaratibu wa kufungwa kwa benki. "Ni jambo lisilowezekana bila kufanya mageuzi katika benki mbili... hili ni jambo la maumivu kwa wa Cyprus, lakini sasa tumepata matokeo ambayo serikali ya Ujerumani iliyasimamia," Schäuble aliwambia wandishi wa habari, na kuongeza kuwa ana uhakika bunge la Ujerumani litaidhinisha mpango huo.

Afisa wa juu aliekuwepo katika mazungumzo hayo alisema Anastasiades alithishia kujiuzulu wakati fulani siku ya Jumapili kama akishinikizwa kupita kiasi. Kiongozi huyo wa kihafidhina, ambaye alikuwa akikabiliana na mgogoro mbaya zaidi kuwahi kuikumba Cyprus tangu uvamizi wa Uturuki mwaka 1974 uliyoigawanya nchi hiyo vipande viwili, alilaazimika kubadilisha msimamo wake wa kuwakingia kifua wamiliki wa akaunti kubwa za amana.

Wanadiplomasia wanasema rais huyo alipigana kulinda mfumo wa biashara wa nchi yake kama kituo cha kifedha kwa wafanyabiashara wa nje, ikivutia viwango vikubwa kutoka matajiri wa Urusi na Uingereza, lakini alishindwa. Umoja wa Ulaya na IMF ziliitaka Cyprus kukusanya kiasi cha euro bilioni 5.8 kutoka sekta yake ya benki kuchangia uokozi wake yenyewe, ili iweze kupatiwa mkopo wa kimataifa wa euro bilioni 10.

Benki ya Cyprus iliyopewa jukumu kushughulikia madeni ya Laiki ambayo inafungwa chini ya makubaliano mapya.
Benki ya Cyprus iliyopewa jukumu kushughulikia madeni ya Laiki ambayo inafungwa chini ya makubaliano mapya.Picha: AFP/Getty Images

Benki kuu yazuia uchukuaji wa viwango vikubwa vya fedha

Huku mabenki yakiwa yamefungwa kwa wiki nzima iliyopita, Benki ya Cyprus iliweka kikomo cha uchukuaji wa fedha kwa euro 100 tu kwa siku kupitia mashine za kutolea fedha (ATM) kwa benki mbili kubwa zaidi ili kuzuia uchukuaji mkubwa wa fedha wa mara moja.

Waziri wa fedha wa Ufaransa Pierre Moscovi alikanusha madai kuwa Umoja wa Ulaya umewakandamiza raia wa Cyprus, akisema ni mfumo wa biashara wa nchi hiyo wa kuvutia fedha za nje uliyoiangusha. "Kwa wale wote wanaosema kuwa tunawakandamiza watu.... Cyprus inaendesha uchumi wa kamari, ambao ulikuwa kwenye kingo za kufilisika," alisema.

Kufuatia taarifa za makubaliano hayo, sarafu ya euro iliimarika dhidi ya dola katika masoko ya fedha ya Asia mapema siku ya Jumatatu. Wachambuzi walikuwa wameonya kuwa kushindwa kufikia kwa makubaliano kungesababisha matatizo katika masoko, lakini baadhi walisema udogo wa kisiwa cha Cyprus ambacho kinachangia asilimia 0.2 tu ya uzalishaji wa kiuchumi katika kanda ya euro ungekuwa na athari ndogo tu.

Mpango uliyowekwa kando wa kutoza kodi kwa amana za benki ulikuwa umewatatiza wawekezaji kwa kuwa uliwakilisha hatua zisizo kifani katika namna Ulaya inavyoshughulikia mgogoro wake wa madeni uliosambaa kutoka Ugiriki hadi Ireland, Ureno Uhispania na Italia.

Waziri wa fedha wa Ureno Vitor Gasper (kushoto), Kamishna wa uchumi na masuala ya fedha wa Umoja wa Ulaya Olli Rehn, na waziri wa fedha wa Cyprus Michalis Sarris.
Waziri wa fedha wa Ureno Vitor Gasper (kushoto), Kamishna wa uchumi na masuala ya fedha wa Umoja wa Ulaya Olli Rehn, na waziri wa fedha wa Cyprus Michalis Sarris.Picha: Reuters

Hali ya shauku

Katika mji mkuu wa Cyprus Nicosia, hali siku ya Jumapili ilikuwa ya shauku. " Sijawahi kuhisi wasiwasi kuhusu mustkabali wa Cyprus tangu nikiwa na miaka 13 na Cyprus ikavamiwa," alisema Dora Giorgali mwenye umri wa miaka 53, mwalimu wa shule ya chekechea aliepoteza kazi yake baada ya kufungwa kwa shule alikokuwa nafundisha. "Nina watoto wanaosoma nje na nawambia wasirudi nchini Cyprus. Hebu fikiria mzazi kusema jambo kama hilo," alisema akiwa katika uwanja mjini Nicosia.

Sekta ya benki ya Cyprus, ambayo ina mali zenye ukubwa wa mara nane zaidi ya uchumi wa nchi hiyo, iliathiriki kutokana na uhusiano wake na Ugiriki, ambako wamiliki binafsi wa dhama walipata hasara ya asilimia 75 mwaka uliyopita.

Bila kufikia makubaliano kufikia mwisho wa Jumatatu, benki kuu ya Ulaya ilisema ingekata fedha za dharura kwa mabenki ya Cyprus, jambo ambalo lingepelekea anguko la sekta hiyo ya benki na pengine kuondolewa kwaCyprus katika knda inayotumia sarafu ya euro.

Bunge la Cyprus lilipopiga kura mara ya kwanza na kuukataa mpango wa awali wa uokozi.
Bunge la Cyprus lilipopiga kura mara ya kwanza na kuukataa mpango wa awali wa uokozi.Picha: AFP/Freier Fotograf

Bunge

Karibu wafanyakazi 200 wa benki waliandamana nje ya ikulu ya rais siku ya Jumapili wakiimba nyimbo za 'troika' (pande tatu za wakopeshaji wa kimataida) nje ya Cyprus" na "Cyprus haitakuwa koloni". Katika kura ya kushangaza siku ya Jumanne, bunge la Cyprus lenywe wajumbe 56 lilikataa pendekezo la kutozwa kodi kwa amana za wateja, wakubwa na wadogo.

Waziri wa fedha Michalis Sarris akatumia siku tatu zisizo na mafanikio mjini Moscow, akijaribu kuishawishi Urusi ambayo raia wake na makampuni wana fedha nyingi katika benki za Cyprus iisaisie nchi hiyo. Siku ya Ijumaa, bunge lilipiga kura kutaifisha mifuko ya pensheni na kutofautisha mabenki mazuri na mabaya - hatua ambayo imetumika kwa benki ya Laiki.

Mabenki ya Cyrus yanayotitia yana amana zinazofikia euro bilioni 68, zikiwemo bilioni 38 katika akaunti za zaidi ya euro 100,000 - viwango vikubwa kwa kisiwa kidogo chenye wakaazi miliomi 1.1, ambacho kisingeweza kuendesha mfumo huo mkubwa wa fedha kivyake.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre, afpe,dpae.
Mhariri: Charo Josephat Nyiro