1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CPJ yaikosoa Tanzania

Lilian Mtono
13 Juni 2018

Shirika la kimataifa linalotetea haki za waandishi wa habari, CPJ limeitaka serikali ya Tanzania kuondoa kanuni zinazolazimisha mitandao ya kijamii kujisajili serikalini katika mchakato mgumu.

https://p.dw.com/p/2zRrY
Symbolbild Cyberkriminalität
Picha: picture-alliance/dpa/O.Berg

Shirika la kimataifa linalotetea haki za waandishi wa habari, CPJ limeitaka serikali ya Tanzania kuondoa mara moja kanuni zinazolazimisha mitandao ya kijamii, blogu na tovuti za kurusha matangazo ya moja kwa moja kujisajili serikalini, katika mchakato ambao unawalazimu kulipa kiasi kikubwa cha fedha za kujiunga pamoja na kukubaliana na kanuni ngumu. 

Katika tamko lake iliyolitoa hii leo, CPJ pia imeitaka serikali ya Tanzania kuondoa vitisho vya kuwachukulia hatua za kisheria watakaoshioshindwa kutimiza matakwa ya kanuni hizo.

Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania, TCRA ilitoa maagizo yaliyoanza kutekelezwa hapo jana, yaliyoagiza tovuti zote kukubaliana na kanuni za maudhui ya mitandao, ama kusitisha uchapishaji. Kulingana na ripoti zilizoandikwa na vyombo vya habari, vilivyonukuu tamko la TCRA, wale wote watakaoshindwa kujisajili hadi ifikapo tarehe 15 ya mwezi Juni watakabiliwa na hatua kali za kisheria.

Kanuni hizo ambazo, awali zilitolewa mwezi Machi mwaka huu na waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo Dkt. Harisson Mwakyembe, ziliweka kiwango kikubwa cha ada ya usajili, ambapo mmiliki wa blogu na mitandao ya mijadala watatakiwa kulipa ada za awali za Dola 484 na ada ya mwaka ya kiasi cha dola 440.

Kulingana na ripoti iliyotolewa na shirika la habari la Reuters mnamo siku ya Jumatatu, tovuti kadhaa, ikiwa ni pamoja na jukwaa maarufu la mijadala nchini humo la Jamii Forums, waliamua kufunga majukwaa yao kwa muda ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya TCRA.

Screenshot Facebook Free Basics
Jamii Forums ni miongoni mwa mitandao mikubwa iliyositisha huduma zake kutokana na hatua hiyo ya serikali.Picha: Facebook

Kulingana na mamlaka hiyo, kushindwa kufikia masharti hayo kunaweza kusababisha wamiliki kuhukumiwa kifungo cha hadi miezi 12 gerezani ama faini ya hadi shilingi milioni 5 za kitanzania ambayo ni sawa na dola, 2,200.

Mratibu wa programu wa CPJ Afrika, Angela Quintal, alipozungumza toka mjini New York Marekani amesema, sera za rais wa Tanzania, John Magufuli kwa kiasi kikubwa zinadidimiza ukakamavu wa vyombo vya habari vya mitandaoni nchini humo, lakini pia Afrika Mashariki kwa ujumla. Amesema sera hii inalenga kukabiliana na malengo ya demokrasia nchini humo. Quintal, amenukuliwa akisema na hapa namnukuu, "Tunazitaka mamlaka kuondoa kanuni hizo mbaya na kuruhusu uhuru wa vyombo vya habari vya mitandaoni kuendelea kustawi", mwisho wa kumnukuu. 

Msemaji wa TCRA Semu mwakanjala, hii leo ameliambia shirika hilo la CPJ kwamba ripoti kuhusiana na gharama kubwa kwenye mchakato wa kujisajili zilikuzwa ama kutiwa chumvi, na kuongeza kuwa serikali ilikuwa ikichukua hatua hiyo ikiwa na kile alichokitaja kama "nia njema ya kuwatambua" watoa huduma za maudhui ya mitandaoni. 

Amesema takriban watoa huduma za maudhui 50 wamekwishajiandikisha tangu kanuni hizo zilipotolewa mwezi Machi. Waziri wa habari, Dkt. Mwakyembe hakuweza kupatikana kwenye simu yake ya mkononi kuzungumzia hatua hiyo.

Mwanzilishi mwenza wa mtandao wa Jamii Forums, Maxence Mello, ameliambia shirika la CPJ kwamba kukubaliana na kanuni hizo kutamaanisha usaliti wa dhamana ya usiri, ambao baadhi ya watumiaji na wanaharakati hutarajia kupewa na  jukwaa hilo.  

Kulingana na taarifa zilizotolewa kwenye tovuti, pamoja na ripoti za Reuters, mchapishaji wa blogu ya The Mikocheni Report, Elsie Eyakuze, ambayo imekuwa ikijiendesha tangu mwaka 2008, mnamo mwezi Mei alitangaza kusitisha huduma zake, kutokana na kanuni hizo mpya.

CPJ, tayari imetoa taarifa za kuongezeka kwa uadui dhidi ya vyombo vya habari nchini Tanzania, tangu rais John Magufuli alipoingia madarakani, ikiwa ni pamoja na kufungiwa kwa magazeti, kupigwa faini kwa vituo vya televisheni pamoja na kupotea kwa mwandishi wa habari za uchunguzi Azory Gwanda.

Mwandishi: Lilian Mtono/CPJ report.

Mhariri:  Josephat Charo