1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia yaongoza kwa mauaji dhidi ya wanahabari

2 Novemba 2015

Kamati ya kimataifa ya kuwalinda waandishi wa habari imesema wanahabari wanapaswa kuwa na hofu zaidi ya kuumizwa, kukamatwa au kuuawa wakati wanapotekeleza majukumu yao.

https://p.dw.com/p/1GyOu
Picha: Harun Ur Rashid Swapan

Kamati hiyo ya kuwalinda wanahabari CPJ imezitaja nchi ambazo mauaji ya waandishi wa habari hakuchukuliwa hatua za kisheria kwa kuwaadhibu wahusika. Sabah al Basi alikuwa akiripoti kutoka Tikrit mwezi Machi mwaka 2011 wakati wanamgambo wa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda walipokuwa wamelidhibiti jengo moja la serikali na kuwazuia mateka waliokuwa ndani ya jengo hilo.

Maafisa wa usalama wa Iraq hatimaye walifanikiwa kudhibiti hali lakini sio bila ya watu hamsini kupoteza maisha yao akiwemo Sabah al Basi. Nani hasa alihusika na kifo cha mwanahabari huyo ni suali ambalo hadi sasa halijaisumbua idara ya mahakama ya Iraq kulitafutia jibu.

Mkurugenzi wa kamati ya kimataifa ya kuwalinda waandishi habari CPJ yenye makao yake mjini New York Marekani Joel Simon amesema hiyo ndiyo halisi nchini Iraq ambapo wanahabari ambao wanafanya kazi zao, wakiripoti kuhusu matukio wanajikuta katika mkumbo wa ghasia na hakuna uchunguzi unaofanywa.

2, Novemba siku ya kukomesha madhila dhidi ya wanahabari

Tarehe 2 Novemba, Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine unaadhimisha siku ya kukomesha visa vya uhalifu dhidi ya wanahabari. Leo ni siku ambayo huadhimishwa kila mwaka kutoa wito kwa uhalifu dhidi ya wanahabari kutofanywa bila ya hatua kuchukuliwa kama mauti yaliyomfika Sabah al Basi.

Mwanahabari wa Urusi Anna Politkowskaja aliyeuawa miaka 8 iliyopita
Mwanahabari wa Urusi Anna Politkowskaja aliyeuawa miaka 8 iliyopitaPicha: picture-alliance/dpa

Simon anasema ana matumaini madogo kuwa waliohusika katika mauaji ya Al Basi watachukuliwa hatua yoyote. Hata hivyo anaitarajia serikali ya Iraq kufanya kila iwezalo kuhakikisha wanahabari nchini humo hawateswi hasa katika maeneo yaliyo chini ya uongozi wa serikali.

Miaka minane iliyopita, kamati ya kuwalinda wahanahabari ilianza kuorodhesha nchi ambazo mauaji ya wanahabari hayachukuliwi hatua za kisheria zinazostahili.

Mkurugenzi huyo wa kamati hiyo ya CPJ anasema kwa mara ya kwanza mwaka huu, Somali ndiyo nchi iliyo na viwango vya juu zaidi vya madhila na mauaji dhidi ya wanahabari bila ya kujali sheria.

Iraq ambayo imekuwa ikiongoza kila mwaka tangu kuanzishwa kwa orodha hiyo miaka minane iliyopita, mwaka huu iko katika nafasi ya pili ikifuatiwa na Syria ambayo inakumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Simon anasisitiza kuwa wauaji wa wanahabari huwa mara nyingi hawaadhibiwi hata katika nchi zilizo na demokrasia kama Mexico, Brazil, Ufilipino, Sri Lanka India na Bangladesh.

Kwa upande mwingine, hatua zimepigwa nchini Urusi katika kesi ya mauaji ya mwanahabari Anna Politkovskaya ambaye alikuwa akiukosoa utawala wa Urusi.

Mwaka jana, Urusi iliwapata wanaume watano na hatia ya mauaji ya mwanahabari huyo, miaka minane baada ya kuuawa nje ya makaazi yake.

Urusi imepiga hatua

Simon anasema hiyo ni hatua iliyopigwa na serikali ya Urusi na kuongeza kuwa baadhi ya waliohusika na kifo chake wamehukumiwa lakini wahusika wakuu bado hawajachukuliwa hatua.

Nembo ya kamati ya kimataifa ya kuwalinda wanahabari CPJ
Nembo ya kamati ya kimataifa ya kuwalinda wanahabari CPJPicha: APTN

Nchi huorodheshwa katika orodha hiyo ya CPJ iwapo kamati hiyo itatambua visa vitano vya mauaji ambayo hayajapatiwa ufumbuzi. Mwaka huu kuna nchi 14 katika orodha hiyo, hiyo ikiwa ongezeko la nchi moja zaidi ikilinganishwa na mwaka jana.

Kote duniani, kamati hiyo imechunguza visa 270 na kugundua kuwa katika visa vingi ni maripota wa nchi husika ambao huuawa kwasababu ya kuandika kuhusu ufisadi.

Wengi wa waandishi hao hukamtwa kabla ya kuuawa na ni nadra sana kuwa wote waliohusika na mauaji ya wanahabari wakiwemo walioamrisha mauaji hayo kuwajibishwa.

Mwandishi: Caro Robi/dw English/http://www.dw.com/en/murders-of-journalists-go-unpunished/a-18819743

Mhariri: Yusuf Saumu