1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Condoleezza Rice kujadili migogoro ya Afrika

3 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CWMA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani,Condoleezza RicePicha: AP

Waziri wa Nje wa Marekani,Condoleezza Rice siku ya Jumanne anaelekea Addis Ababa,Ethiopia kushauriana na viongozi na mawaziri wa kanda hiyo,katika juhudi ya kupunguza mivutano na migogoro ya Pembe ya Afrika,Maziwa Makuu na Sudan.

Wakati wa ziara hiyo,Rice atakutana na viongozi wa Uganda, Rwanda,Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kujadili matatizo yanayokabili eneo la Maziwa Makuu.Majadiliano hayo yanatazamiwa kushughulikia miradi ya usalama ya hivi sasa,ikiwa ni pamoja na mpango wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Rwanda kuwanyanganya silaha wapiganaji wa FDLR- kundi lililohusishwa na mauaji ya kiholela ya Watutsi nchini Rwanda katika mwaka 1994.

Mzizi mwingine wa machafuko ni Jemadari muasi Laurent Nkunda anaedai kuwa anawalinda Watutsi walio wachache.Tangu mwisho wa mwezi Agosti,jimbo la machafuko la Kivu ya Kaskazini limeshuhudia mapambano makali kati ya kama waasi 4,000 walio watiifu kwa Nkunda na zaidi ya wanajeshi 20,000 wa serikali ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,Laurent Kabila.

Hata kundi la waasi kutoka Uganda LRA linalojificha nchini Kongo linachangia machafuko. Naibu wa Waziri wa Nje wa Marekani anaeshughulikia masuala ya Afrika,Jendayi Frazer amesema,mkutano wa kilele siku ya Jumatano, utazingatia mkakati wa kanda hiyo unaoungwa mkono na Marekani kwa matumaini kuwa utasaidia kuimarisha uwezo wa Kongo kukabiliana na makundi yanayochafua utulivu.

Wakati wa ziara yake ya siku mbili,Condoleezza Rice atajadili pia mgogoro wa Somalia katika Pembe ya Afrika,nchi inayojikuta vitani tangu mwaka 1991.Lakini maoni ya jumuiya ya kimataifa yanatofautiana katika suala la kupeleka Somalia vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa ili kuleta utulivu nchini humo.Licha ya wanamgambo wa makundi yenye itikadi kali za Kiislamu kutimuliwa na majeshi ya Ethiopia miezi 10 iliyopita, machafuko yangali yakiendelea nchini Somalia. Ethiopia ilipeleka vikosi vyake kuisaidia serikali ya mpito ya Somalia.

Katika jitahada ya kutafuta suluhisho,Rice atakutana na Rais wa Somalia Abdullahi Yusuf Ahmed na Waziri Mkuu mpya wa Somalia Nur Hassan Hussein.Mkutano huo utahudhuriwa pia na wajumbe wa Umoja wa Afrika,Umoja wa Mataifa,Uganda, Djibouti na Ethiopia.

Mada nyingine itakayoshughulikiwa na Rice wakati wa ziara yake ya siku mbili nchini Ethiopia ni ule Mkataba wa Amani wa mwaka 2005 uliotiwa saini kati ya serikali ya Khartoum ya Rais Omar el-Beshir na Sudan ya Kusini.Mvutano mpya uliozuka kati ya Ethiopia na Eritrea vile vile ni suala litakalojadiliwa na waziri Condoleezza Rice atakapokutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi.