1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Colombia yasaini makubaliano ya kihistoria

24 Septemba 2016

Colombia itafunguwa ukurasa mpya katika mzozo wa nusu karne ambao umeitia doa la umwagaji damu historia yake ya sasa wakati kundi la waasi la FARC na serikali zitakapotia saini makubaliano ya amani Jumatatu (26.09.2016).

https://p.dw.com/p/2QYJe
Kolumbien FARC Friedensvertrag
Picha: picture-alliance/dpa/M. Duenas Castaneda

Rais Juan Manuel Santos na kiongozi wa waasi wa kundi linalojiita Jeshi la Mapinduzi la Colombia (FARC)  Rodrigo Londono ambaye anatambulika zaidi kwa jina lake la utani Timoleon "Timochenko" Jiminez watatia saini makubaliano hayo sasa kumi na moja jioni katika hafla ilioandaliwa kufanyika katika mji wa zama za ukoloni wenye uchangamfu wa Cartagena ulioko katika mwambao wa Caribbean.

Hafla hiyo itaanza kwa kutowa heshima kwa jeshi na polisi wa Colombia ikiongozwa na Santos na kutakuwepo ibada ya maombi ya amani na usuluhishi itikayofanyika katika Kanisa Katoliki la karne ya 18 lilioko katika mji wa kale wa Cartagena.

Miongoni mwa wageni watakaohudhuria ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon,Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na kundi la viongozi wa Amerika Kusini akiwemo Rais Raul Castro ambaye nchi yake ndio iliokuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani yaliyodumu kwa miaka minne ambayo ndio yaliyozaa makubalino ya mwisho hapo Augusti 24.Washiriki 25,000 walioalikwa kuhudhuriwa wametakiwa wavalie mavazi meupe.Hafla hiyo inafanyika kabla ya hatua ya mwisho ya kuridhiwa kwa makubaliano hayo.

Makubaliano kupigiwa kura ya maoni

Viongozi wa FARC katika mkutano wao wa mwisho kama waasi.
Viongozi wa FARC katika mkutano wao wa mwisho kama waasi.Picha: picture-alliance/dpa/R.Mazalan

Wananchi wa Colombia watayapigia kura makubaliano hayo katika kura ya maoni iliopangwa kuitishwa hapo Oktoba pili . Uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni umeonyesha kwamba wale wenye kuunga mkono wa kura ya "Ndio" wanaongoza.

Kundi la FARC la wapiganaji wa chini kwa chini wa Kimarxist lilianzisha vita dhidi ya serikali ya Colombia hapo mwaka 1964 baada ya uasi wa wakulima uliozimwa kwa kutumia ukatili na jeshi.Kwa miongo mingi mzozo huo umekuja kuyajumuisha makundi kadhaa ya waasi wa sera za mrengo wa kushoto, wanamgambo wa mrengo wa kulia na magenge ya madawa ya kulevya na kuacha haiba ya vifo na uharibifu : zaidi ya watu 260,000 wameuwawa ,45,000 hawajulikani walipo na milioni 6.9 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao.

Akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hivi karibuni baada ya kukabidhi makubaliano hayo ya amani yenye kurasa 297 yakiwa yamefungwa ndani ya bendera ya Colombia ya rangi ya njano,buluu na nyekundu Rais Santos amesema wanaugeuza ukarasa wa vita na kuandika ukurasa mpya wa amani.

Waasi waridhia kwa kauli moja

Waasi wakishangilia makubaliano ya kihistoria.
Waasi wakishangilia makubaliano ya kihistoria.Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Mazalan

Wajumbe wa FARC kwa kauli moja waliridhia makubaliano hayo Ijumaa katika mkutano wa taifa huko El Diamante eneo lilioko mbali na ngome ya jadi ya kundi hilo kusini magharibi mwa Colombia.Mjumbe wao mkuu wa amani Ivan Marquez alitangaza "Vita vimekwisha " na kushangiliwa na wajumbe wa waasi waliokuwa wamevalia kiraia.Ikiwa mambo yote yatakwenda kama ilivyopangwa huo utakuwa mkutano wa mwisho wa FARC kama kundi la wapiganaji.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo kundi hilo linatazamiwa kuzinduliwa upya kama chama cha kisiasa.Makubaliano hayo yanajumuisha pia kupatiwa haki na kulipwa fidia kwa wahanga wa mzozo huo,mageuzi ya ardhi,,kusalimisha silaha,kupambana na madawa ya kulevya ambayo yamechochea matumizi ya nguvu katika nchi hiyo yenye kuzalisha mihadarati kwa wingi duniani halikadhalika kuyafuatilia na kutekeleza makubaliano hayo.

Makubaliano hayo yanatowa msamaha kwa "uhalifu wa kisiasa " uliotendeka wakati wa mzozo huo lakini sio ule ukatili kubwa sana kama vile mauaji,mateso na ubakaji.

Mwandishi: Mohamed Dahman / AFP

Mhariri: Bruce Amani