1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton ziarani Russia

13 Oktoba 2009

Clinton anataka aungwe mkono na Russia juu ya suala la Iran

https://p.dw.com/p/K56L
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Bibi Hillary Clinton, akipokewa na mwenzake wa Russia, Sergey Lavrov, kwa mazungumzo mjini MoskoPicha: AP

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Bi Hillary Rodham Clinton, jana usiku amewasili nchini Urusi katika mfululizo wa ziara yake barani Ulaya.

Bi Clinton aliwasili Moscow akitokea mjini Belfast Ireland ya Kaskazini.

Hii ni ziara ya kwanza ya Bi Clinton nchini Urusi akiwa kama mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani, ambapo pia ni kituo cha mwisho cha ziara yake ya siku tano barani Ulaya.

Akiwa nchini humo, Hillary Clinton amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov, na baadaye pia atakutana na rais wa nchi hiyo Dmitry Medvedev, katika harakati za kutafuta uungwaji mkono na serikali ya Moscow, kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran.

Akizungumzia juu ya suala la silaha za nyuklia rais Medvedev

alisema:

 "mkataba wa kupunguza silaha za kimbinu unamalizika Disemba 5, kimsingi tumewapa maagizo washauri wetu, wamalize mazungumzo yao hadi wakati huo."

Baada ya kuchaguliwa kwa Barack Obama kuwa rais wa Marekani, pande zote zimekuwa zikitafuta namna ya kusonga mbele, kutoka katika mfululizo wa migongano ya kidiplomasia iliyotia dosari uhusiano wa nchi hizo mbili katika miaka iliyopita, wakati ambapo Moscow inaonekana kuwa mdau muhimu katika mchakato wa nyuklia wa Iran.

Bi Clinton amewaambia waandishi wa habari, jinsi alivyosikitika kwa kushindwa kwake kuzuru Urusi mnamo mwezi wa Julai kutokana na kuugua, wakati Rais Barack Obama alipofanya ziara ya mazungumzo na Rais Medvedev.

US-Präsident Barack Obama und der russische Präsident Dmitry Medvedev
Rais Barack Obama wa Marekani(kulia) na Rais Dmity Medvedev wa RussiaPicha: AP

Alisema kwa kuwa sasa amepona, na uhusiano wa Marekani na Urusi ukiwa unaimarika, kilichobaki ni kusonga mbele ili kutimiza malengo.

Maafisa wa Marekani wanasema kuwa, Bi Clinton ambaye alishauriana na mshirika wake mkubwa Uingereza juu ya suala la Iran, anataka kufahamu ni mbinyo wa kiasi gani Urusi imejiandaa kutoa kwa pamoja na washirika wengine, endapo Iran itashindwa kuwajibika juu ya suala lake la mpango wa nyuklia.

Maafisa hao wamesema pamoja na mambo mengine, suala la kuwekwa vikwazo vikali zaidi, litajadiliwa kwa kirefu kama sehemu ya mbinyo kwa Iran.

Marekani, Urusi, China, Uingereza, Ufaransa, ambazo ni wajumbe wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani, zinaitaka Iran isitishe mpango wake unaopingwa vikali wa urutubishaji wa madini ya uranium.

Mataifa ya magharibi yana wasiwasi kuwa mpango huo wa urutubishaji wa madini ya Uranium, unalenga katika kutengeneza bomu la nyuklia, jambo ambalo serikali ya Tehran imelipinga vikali, na inasema kuwa mpango huo ni kwa matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.

Marekani, Ufaransa na Uingereza, ziliweka hadharani wasiwasi wao juu ya dhamira ya Iran, baada ya kugundua mwishoni mwa mwezi uliopita, mtambo wa pili wa urutubishaji wa uranium uliojengwa kwa siri, karibu na mji mtakatifu wa Qom.

Rais wa Urusi Dmitry Medvedev, mwezi uliopita aliipa matumaini ya ushirikiano serikali ya Marekani, pale aliposema kuwa, katika mazingira kama hayo ya kujengwa kwa mtambo wa siri, vikwazo haviwezi kuepukika.

Duru za Marekani zimeongeza kuwa, Hillary Clinton angependa pia kujadiliana juu ya Iran kuuhamishia mtambo huo nchini Urusi kwa ajili ya urutubishaji, hatua ambayo itaondoa wasiwasi wa dhumuni la urutubishaji huo.

Mwandishi:Lazaro Matalange/AFP

Mhariri: Miraji Othman