1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton, Trump wazungumzia uchumi

Bruce Amani
5 Novemba 2016

Mgombea wa urais Marekani kwa tikiti ya Democratic Hillary Clinton na mwenzake wa Republican Donald Trump walikabiliana kuhusu uimara wa uchumi katika mkondo wa mwisho wa kinyang'anyiro chao cha Ikulu ya White House

https://p.dw.com/p/2SCKu
USA Vorwahlen Bildkombo Donald Trump Hillary Clinton
Picha: Reuters/D. Becker/N. Wiechec

Zikiwa zimesalia siku nne katika kinyang'anyiro hicho kikali ambacho kiliimarika zaidi katika wiki iliyopita, kila mgombea alimshambulia mwenzake kuwa asiyefaa kuwa rais wa Marekani katika hatua ya mwisho ya kusaka kura katika majimbo muhimu ambayo huenda yakaamua matokeo ya uchaguzi huo wa Jumanne wiki ijayo.

Clinton anaongoza dhidi ya Trump kwa tofauti ya asilimia 5, kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi wa pamoja wa Reuters na Ipos yaliyotolewa Ijumaa, na kudumisha uongozi wake katika utafiti wa kitaifa hata wakati kinyang'anyiro kikiwa kikali kabisa katika majimbo muhimu ambayo kura hukaribiana.

Katika uchunguzi wa maoni uliofanywa kati ya Oktoba 30 na Novemba 4, asilimia 44 ya Wamarekani wanaoweza kupiga kura walimuunga mkono Clinton wakati asilimia 39 wakimuunga mkono Trump.

Bill Clinton na mkewe Hillary katika mojawapo ya kampeni za Democratic
Bill Clinton na mkewe Hillary katika mojawapo ya kampeni za mgombea huyo wa DemocraticPicha: Getty Images/J. Sullivan

Akizungumza katika tamasha la muziki mjini Cleveland lililohudhuriwa na wasanii maarufu akiwemo Jay Z, Clinton alisema "tuna kazi iliyobaki ya kufanya, vizingiti zaidi vya kuvunja, na kwa msaada wenu, tutaweza kumaliza kabisa”.

Katika mkutano wake wa mwisho wa hadhara siku ya Ijumaa jimboni Pennsylvania, Trump alimkejeli Clinton. "niko hapa peke yangu. Mimi tu, hakuna gitaa, hakuna piano, hakuna chochote”. Alisema.

Mapema, katika mkutano mjini Pittsburgh, Clinton alitaja ripoti ya ya karibuni ya serikali kuhusu ajira kuwa ni ushahidi wa uchumi uko imara. Ripoti hiyo ilionyesha kipato cha juu kwa wafanyakazi pamoja na kuwapo nafasi za kazi 161,000 katika mwezi Oktoba na kupungua kwa kiwango cha ukosefu wa ajira hadi asilimia 4.9 kutoka asilimia 5. "naamini uchumi wetu utafanya vyema zaidi. Wakati tabaka la wastani linanawiri, Marekani inanawiri”. Alisema Clinton.

Melania Trump, mke wa mgombea wa Republican Donald Trump
Melania Trump, mke wa mgombea wa Republican Donald Trump akimpigia debe katika mkutano wa kampeniPicha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Trump alipinga mtazamo huo wa Clinton, akiuambia umati jimboni New Hampshire kuwa ripoti hiyo ya ajira ni "janga kubwa kabisa” na imeegemea zaidi kwa idadi kubwa ya watu ambao wameacha kutafuta kazi na hawako tena katika soko la ajira.

"Hakuna anayeamini takwimu hizi. Takwimu hizi zilizotolewa ni za ulaghai”. Alisema, akimaanisha takwimu zilizotolewa na Wizara ya Kazi ya Marekani.

Uchumi na maono yanayoshindana ya wagombea hao katika siku za usoni huenda yakawa mambo muhimu katika kuubadilisha uamuzi wa wapiga kura katika majimbo yanayoyumba ya Ohio, Pennsylvania na Michigan.

Wagombea wote walifanya mikutano Ohio na Pennsylvania Ijumaa, ambapo Trump alikuwa New Hampshire na Clinton akaongeza moja jimboni Michigan. Kila moja ya majimbo hayo ni muhimu katika harakati za jimbo hadi jimbo kwa ajili ya kura 270 za uchaguzi zinazohitajika kushinda urais.

Mwandishi: Bruce  Amani/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga