1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton na Trump wazuliana tena kashfa

20 Oktoba 2016

Dakika za lala salama zinashuhudiwa nchini Marekani huku wapinzani katika uchaguzi huo, Donald Trump na Hillary Clinton, wakikutana tena kwa mara ya tatu na ya mwisho katika mdahalo wa televisheni huko Las Vegas.

https://p.dw.com/p/2RTKr
USA | Ende der 3. Präsidentschaftsdebatte 2016 in Las Vegas
Picha: picture-alliance/dpa/G. He

Katika mdahalo wa mwisho uliorushwa moja kwa moja na vituo kadhaa vya televisheni usiku wa Jumatano (19 Oktoba), Trump alidai kuwa wafuasi wa Clinton wanapanga kuiba kura kwenye uchaguzi. Na alipoulizwa iwapo atakubali matokeo ya uchaguzi huo wa Novemba 8, alisema: ''Nitajibu wakati huo, kwa sasa sitasema kitu.''

Clinton alitangaza kuwa ameshtushwa na majibu hayo yanayoonekana kuwa mashambulizi dhidi ya miaka 240 ya demokrasia nchini Marekani. Akimnukuu aliyekuwa mpinzani wake katika kuwania tiketi ya chama cha Democrat, Bernie Sanders, alimtaja Trump kuwa mtu hatari zaidi kuwahi kuwania urais wa nchi hiyo katika historia ya sasa ya Marekani.

Trump alifika katika mdahalo huo wa tatu akiwa na matarajio ya kudumisha matumaini ya kampeni yake siku 20 kabla ya uchaguzi. Huku akikabiliwa na ukosoaji wa kimaadili katika masuala ya kimapenzi na kupoteza ushawishi katika majimbo muhimu, Trump alijaribu kutumia nafasi hiyo ya mwisho kuwashawishi wapiga kura.

Alisema kuwa vyombo vya habari havina ukweli na ni sehemu ya mfumo wa kifisadi huku akigusia ripoti za wanawake waliomshtumu kwa dhulma za kimapenzi alizozitaja kuwa shutuma za kupangwa zinazopigiwa upatu na Clinton.

Aliongeza kuwa mamilioni ya wapiga kura bandia wamesajiliwa na kwamba Clinton hangepaswa kuruhusiwa kuwania urais huo kwa sababu alishughulikia vibaya barua pepe za wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya Marekani.

US TV Debatte Trump vs Clinton
Wagombea urais katika mdahala wa mwisho kabla ya uchaguziPicha: Reuters/L. Nicholson

Clinton amkosoa Trump kutumika na Putin

Wakati huo huo, Clinton alimkosoa Trump na kudai kuwa Rais Vladimir Putin wa Urusi anamuunga mkono katika kinyang’anyiro hicho. Clinton alitaja ripoti kutoka kwa taasisi za ujasusi za Marekani kuwa udukuzi wa intaneti uliofanywa na Urusi ulikuwa umelenga chama chake na kampeni zake na kutaka Trump alaani udukuzi huo.

Hata hivyo, Trump alijipigia debe kuwa katika nafasi bora zaidi ya kujadiliana kuhusu uhusiano mwema na Urusi kuliko Clinton na kwamba Putin hamuheshimu Clinton, suala lililojibiwa kwa haraka na Clinton kwamba "ni kwa sababu angependelea kushirikiana na kikaragosi kama rais wa Marekani."

Majibazano hayo ni moja tu kati ya msururu wa majibizano kati ya wagombeaji hao wawili kuhusiana na masuala mengi kama vile uhamiaji na suala la hali ya Syria.

Wakati mmoja, Trump alikatiza maelezo ya Clinton na kumtaja kuwa mwanamke muovu.

Wagombeaji hao waliondoka katika jukwaa bila ya kusalimiana.

Mwandishi: Tatu Karema/DPA,AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo