1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton ataka Assad abanwe zaidi

Admin.WagnerD20 Aprili 2012

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton amelitaka Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuiwekea Syria vikwazo vya silaha na kiuchukulia hatua nyingine kali ili kusitisha umwagaji damu unoendelea nchini humo

https://p.dw.com/p/14iFa
Waiziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Alain Juppe akinena na mwenzake wa Marekani, Hillary Clinton
Waiziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Alain Juppe akinena na mwenzake wa Marekani, Hillary ClintonPicha: Reuters

Matamshi ya Clinton yamekuja wakati ambapo katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon anamlaumu rais Bashar Assad kwa kushindwa kuheshimu mpango wa amani ulioanza kutekelezwa wiki iliyopita.

"Tunahitaji kunendeleza kazi na kuelekeza nguvu zetu kwenye kupata ruhusa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili tupate mamlaka ya kusonga mbele muda utakapowadia," alisema Clinton

Hotuba ya Clinton ilijikita katika pendekezo la Marekani la kulitaka kundi la marafiki wa Syria kuandaa mkakati wa dharura endapo mpango wa amani wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ulioandaliwa na mjumbe maalumu Koffi Annan utashindwa kufikia lengo.

Wandamanaji wa mrengo wa kushoto nchini Uturuki wanamuunga mkono rais Assad
Wandamanaji wa mrengo wa kushoto nchini Uturuki wanamuunga mkono rais AssadPicha: Reuters

Ingawa Marekani inatambua kwamba uwezekano wa kumuondoa Assad kwa sasa ni mdogo, azimio la Umoja wa Mataifa analolitaka Clinton linaweza kuwaongezea nguvu waasi wanaopambana na serikali yake.

Alisema kinachotakiwa kwa sasa ni kuongeza shinikizo kwa baraza la Usalama ili kuandaa rasimu ya azimio la vikwazo zaidi ikiwa ni pamoja na vya usafiri, fedha, silaha vitakavyolaazimisha utawala wa Assad kutekeleza hatua sita za mpango wa Annan.

Hofu ya kura ya turufu
Lakini jaribio lolote la vikwazo vya Umoja wa Mataifa litakumbana na upinzani kutoka kwa washirika wa Syria, Urusi na China ambazo zina kura za turufu katika Baraza la usalama. Tayari Urusi na China zimepiga turufu dhidi ya maazimio mawili ya Umoja wa Mataifa kulaani utawala wa Assad.

Clinton alisema amezungumza na waziri wa mambo ya Nje wa Urusi, Sergio Lavrov na kumueleza kuwa hali iliyoko nchini Syria inazidi kudorora.

Wandamanaji nchini Syria wakiwa wamebeba mabango yanayozikosoa China na Urusi
Wandamanaji nchini Syria wakiwa wamebeba mabango yanayozikosoa China na UrusiPicha: dapd

Naye waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague alisema: "Kama hatua ya kusitisha mapigano haileti ufanisi na mpango wa Annan haufuati, basi ni wazi kwamba anayehusika ni serikali ya Syria na ndiyo maana tunaipia urusi jukumu la kuishinikiza serikali hiyo kutekeleza."

Msimamo wa Urusi
Lakini Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergio Levrov amesema pamoja na kuwepo ukiukaji mdogo, lakini hatua ya kusitisha mapigano ilikuwa na ufanisi na kuongeza kuwa jukumu la kulinda haki za binadamu, usalama na uhuru wa nchi viko mikononi mwa Syria wenyewe.

Mnamo wiki za hivi karibuni, Urusi imekuwa ikimkosoa mshirika wake Assad kutokana na hali inayozidi kuwa mbaya nchini humo, lakini wakati huo huo imeyakosoa pia mataifa ya kigeni kwa kuwaunga mkono wpinzani nchini Syria.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE\AFPE
Mhariri:Mohammed Abdul Rahman