1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chombo cha Umoja wa Mataifa chapendekeza mpango wa kupambana na mzozo wa chakula duniani.

Mohmed Dahman24 Mei 2008

Mbegu zaidi na zilizo bora,mbolea,umwagailiaji maji katika mashamba na vifaa vya usafiri ni vitu vinavyohitajika kupambana na uhaba wwa chakula duniani kote.

https://p.dw.com/p/E5FS
Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP likigawa chakula nchini Angola.Picha: WFP

Hilo ni pendekezo la mpango wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa ECOSOC kupambana na uhaba wa chakula duniani ili kusaidia mamilioni ya watu wanaohangaika kujipatia chakula cha kutosha wakati bei za vyakula zikiendelea kupanda.

Kwa mujibu wa taarifa iliowekwa kwenye tovuti ya shirika hilo Rais wa ECOSOC Leo Merores ameuambia mkutano maalum wa kikao hicho cha wanachama 52 kwamba kuongezeka sana kwa bei za vyakula na uhaba wa chakula kunaathiri afya na kuendelea kuwa hai kwa mamilioni ya watu duniani.

Kwa mujibu wa repoti ya ECOSOC kwenye tovuti yake katika kipindi cha miaka miwili iliopita bei za bidhaa za vyakula duniani zimeongezeka mno huku bei ya mchele ikipanda zaidi ya maradufu tokea mwishoni mwa mwezi wa Januari mwaka huu.

Merores amesema katika taarifa kwamba katika kipindi cha muda mfupi baraza hilo la Umoja wa Mataifa linakusudia kuwasaidia wakulima kukidhi mahitaji yao ya uzalishaji wa mazao katika msimu ujao wa upandaji wa mazao.

Pia ametaka kuwepo na haja ya dharura katika kukamilisha mazungumzo ya biashara ya Duru ya Doha ambayo yanapaswa kutatuwa tatizo la ruzuku za kilimo na ushuru la nchi zilizoendelea kwa nia ya kusaidia maendeleo ya kilimo katika nchi za kimaskini.

Mazungumzo ya Duru ya Doha ya Shirika la Biashara Duniani kwa ajili ya kufikia makubaliano ya biashara duniani yalianzishwa hapo mwaka 2001.

Mikutano iliofanyika mjini New York wiki iliopita ilikiwa imesanifiwa ili kutumika kama daraja kati ya mkutano uliomalizika hivi karibuni wa Kamisheni ya Maendeleo Endelevu na Mkutano wa Viongozi juu ya Chakula uliopangwa kufanyika mjini Rome Italia katika kipindi kisichozidi wiki mbili.

Katika mkutano huo wa Rome viongozi wa serikali na mawaziri watatafuta njia za kuzuwiya mamilioni zaidi ya watu kutumbukia kwenye njaa.

Wakati huo huo Saudi Arabia imetowa mchango wa dola nusu bilioni kwa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP kusaidia kupambana na ongezeko la bei za chakula duniani na imeliwezesha shirika hilo kufikia lengo la lake la mchango wa dola 755 milioni.

Shirika hilo limesema katika taarifa kwamba bei za juu za vyakula zinawakilisha changamoto kubwa kabisa kuwahi kukabiliwa na shirika hilo la WFP katika historia yake ya miaka 45 huku watu milioni 130 wakiwa hatarini kutumbukia kwenye dimbwi la njaa.

Mkurugenzi mtendaji wa WFP Josette Sheeran amesema fedha hizo zitasaidia kufidia gharama za chakula na mafuta ambazo zimeongezeka sana katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na zitafanikisha mipango ya chakula inayohitajika mno barani Afrika na katika sehemu nyengine duniani.Sheeran amesema msaada huo wa Saudi Arabia utasaidia kuzuwiya watu wengi wasipoteze maisha na wengine wasikumbwe na utapia mlo na maradhi na hata pia kusaidia kuzima machafuko ya kiraia.

Michango inaliwezesha shirika la WFP kuendelea kutowa chakula kwa mamilioni ya watoto walioandikshwa shule na mipango ya maarifa ya kutibu magonjwa kwa ulishaji wa chakula nchini Kenya, Yemen,Ethiopia na Somalia na sehemu nyengine nyingi zinazokabiliwa na njaa.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia bei za vyakula zimeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka mitatu na kuchochea ghasia nchini Misri na Haiti na maandamano katika nchi nyengine na kupigwa marufuku usafirishaji nje wa chakula kutoka Brazil, Vietnam, India,Misri na hivi karibuni Tanzania.

Rais wa Benki ya Dunia Robert Zoellick amesema watu bilioni mbili duniani kote wanataabika kutokana na bei za juu za vyakula na watu wengine milioni 100 yumkini wakazidi kuzama kwenye dimbwi la umaskini kutokana na mzozo huo wa chakula.