1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yatazamia ukuaji wa uchumi

M.von Hein - (P.Martin)9 Machi 2009

Uchumi wa China hauna matatizo ya mikopo,lakini athari za mzozo wa fedha duniani zinadhihirika katika sekta ya mauzo.Hata hivyo, wanasiasa waliokusanyika Beijing kwenye kikao kikuu cha bunge la taifa wana matumaini mema.

https://p.dw.com/p/H8jf
Chinese Premier Wen Jiabao, bottom, is applauded as he delivers his work report during the opening session of the National People's Congress in Beijing's Great Hall of the People Thursday, March 5, 2009. China opened the annual session of its legislature Thursday, its first since the global financial meltdown started last year. (AP Photo/Greg Baker)
Waziri Mkuu wa China Wen Jiabao akihutubia kikao cha Bunge la Taifa mjini Beijing.Picha: AP

Bunge la taifa la China lenye wabunge 3,000 hukutana mwaka mara moja kwa majuma mawili mjini Beijing.Kwa kweli huko si mengi yanayojadiliwa kwani maamuzi yanapitishwa kwengine hapo kabla.Lakini huko ndio viongozi wa serikali hutoa hotuba zao ndefu.Kwa mfano Waziri Mkuu wa China Wen Jiabao alihutubia kwa saa mbili nzima alipofungua kikao cha bunge siku ya Alkhamisi.Akaeleza kuwa athari za mzozo wa fedha duniani zilianza kudhihirika nchini China tangu Septemba mwaka jana. Amesema,mwaka huu wa 2009 utakuwa wakati mgumu sana,lakini serikali itatumia pesa zaidi kusaidia kufufua uchumi nchini humo.

Waziri Mkuu Wen anatabiri kuwa uchumi mwaka huu utakuwa kwa asilimia 8.Na kama inavyoaminiwa na wengi ukuaji wa asilimia 8 ndio unaohitajiwa kutoa nafasi za ajira za kutosha.Kwa hivyo wachambuzi wanahisi kuwa lengo la tarakimu zilizotajwa na Wen ni kuwatia moyo wananchi. Hata Gavana wa Benki Kuu ya China Zhao Xiaochuan alipozungumza na waandishi wa habari aliashiria maendeleo katika sekta ya uchumi.Alisema:

"Takwimu zinaonyesha kuwa katika baadhi ya sekta, uchumi utatulia na utaimarika.Hiyo huonyesha kuwa sera za kufufua hali ya uchumi zinafanya kazi.Baraza la taifa lilieleza kinagaubaga kuwa mzozo wa kiuchumi unapaswa kukabiliwa haraka na kwa pamoja."

Wachina wanahitaji kutiwa moyo hata kama China haipambani na mizozo ya benki kwani mfumo wake wa benki haukuathirika moja kwa moja kwa mzozo wa fedha duniani.Lakini uchumi halisi umeathirika sana kama anavyoeleza Doris Fischer,mtaalamu wa masuala ya China katika taasisi ya Kijerumani inayohusika na sera za maendeleo. Anasema,China imeathirika katika sekta ya maagizo na mauzo.Bidhaa za China hasa huuzwa katika nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda.Na sasa maagizo ya nchi hizo yamepunguka kwa hivyo uchumi wa China unaathirika.

Kwani upungufu wa maagizo umesababisha viwanda kufungwa nchini China na idadi ya wakosa ajira kuongezeka.Hiyo ni hali inayosababisha wasiwasi nchini China kuwa hatimae huenda ikachochea matatizo ya kijamii na kisiasa kwani mafanikio ya kiuchumi ndio husaidia kwa sehemu kubwa kuimarisha utulivu wa kisiasa nchini humo.