1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yapata kiongozi mpya

15 Novemba 2012

Chama tawala cha kikomunisti nchini China kimemchagua Katibu Mkuu wake mpya Xi Jinping na kufichua majina ya viongozi wengine saba watakaoongoza taifa hilo.

https://p.dw.com/p/16jWg
Xi Jinping Vize Präsident ChinaPicha: Reuters

Xi Jinping amepata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliofanyika jana kuchukua nafasi hiyo pamoja na ya mkuu wa majeshi katika taifa hilo ambalo kwa sasa linakabiliwa na changamoto za rushwa pamoja na hali ya wasiwasi kuhusu uchumi. Yeye ndiye pia atakayekuwa rais wa nchi hiyo. MKutano huo umemchagua Li Kegiang kuwa naibu wa Jinping.

Pamoja na uteuzi huo, chama hicho pia kimelitangaza baraza lenye wajumbe saba kutoka pande zote mbili za wahafidhina na wale wanaopendelea mabadiliko ya uchumi ambao ndio watakaoiongoza China kwa miaka kumi ijayo.

Idadi hiyo imepunguzwa kutoka tisa wa awali ambayo wachambuzi wanasema itarahisisha mchakato wa kufanya maamuzi ndani ya chama yanayohusu masuala nyeti ya taifa hilo kwa miaka 10 ijayo ukizingatia kuwa nchi hiyo inapitia mabadiliko ya haraka.

Xi Jinping kiongozi mpya wa China
Xi Jinping (wa kwanza) kiongozi mpya wa ChinaPicha: Reuters

Siku ya Jumatano chama hicho kilichagua kamati kuu yenye wajumbe 200 ambao ndio waliochagua safu hiyo ya uongozi wa juu wa watu saba.

Akihutubia wajumbe wakati wa kufungwa kwa mkutano huo Xi amesema kuwa anafahamu kiu ya wananchi ya kupata maisha bora lakini akaonya juu ya changamoto mbalimbali ambazo zinazidi kuongezeka kila kukicha.

Xi amesema na hapa ninamnukuu, "Chama chetu kimejikita katika kuhudumia wananchi. Kimewaongoza wananchi kupata mafanikio makubwa ambayo yanasifika duniani na tunakila sababu ya kujivunia mafanikio haya." mwisho wa kumnukuu.

Li Keqiang Naibu wa Xi Jinping
Li Keqiang Naibu wa Xi JinpingPicha: Reuters

Kiongozi huyo ameongeza kuwa kamwe hawatalewa na mafanikio hayo nakwamba hawatabweteka kutokana na vyeo hivyo kwa kuwa chama kinakabiliwa na changamoto kubwa na kina matatizo makubwa yanayohitaji kushughulikiwa.

Xi mwenye umri wa miaka 59 ana uwezo mkubwa wa masuala ya siasa akiwa ni mtoto wa Luteni katika utawala wa kiongozi wa mapinduzi Mao Zeodong. Atakalia rasmi kiti chake kipya mwezi Machi mwakani atakapokabidhiwa kutoka kwa mtangulizi wake Hu Jintao. Kipindi hicho ndio wakati ambao chama tawala kitakapothibitisha kuchaguliwa kwake.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanajaribu kuangalia safu ya uongozi ilivyo ili kujua ni upi kati ya upande wa wahafidhina na wanamageuzi una nguvu sana, lakini wanasisitiza kwamba utulivu bado utaendelea kutawala siasa za chama hicho cha kikomunisti.

Safu ya viongozi saba wapya wa China
Safu ya viongozi saba wapya wa ChinaPicha: Reuters

Japan ambayo inazozana na China imesema inataka kujenga mahusiano mazuri na uongozi mpya. Kauli hiyo ya Japan inatokana na mzozo uliopo baina ya mataifa hayo unaohusiana na safu ya visiwa katika eneo la mashariki ya bahari ya China ambao umeyaweka mahusiano ya majirani hayo katika hali isiyo nzuri.

Mwandishi: Stumai George/AFP/Reuters

Mhariri: Hamidou Oummilkheir