1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaipa Afrika mkopo wa dola bilioni 20

19 Julai 2012

Rais wa China Hu Jintao leo ametangaza mkopo wa dola Bilioni 20 kwa nchi za bara la Afrika katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, na kuimarisha uhusiano uliopo kati ya nchi hiyo na Afrika.

https://p.dw.com/p/15am5
Source News Feed: EMEA Picture Service ,Germany Picture Service China's President Hu Jintao delivers a speech during the opening ceremony of the Fifth Ministerial Conference of the Forum on China-Africa Cooperation (FOCAC) at the Great Hall of the People in Beijing, July 19, 2012. Hu on Thursday offered $20 billion in loans to African countries over the next three years, boosting a relationship that has been criticised by the West and given Beijing growing access to the resource-rich continent. REUTERS/Jason Lee (CHINA - Tags: POLITICS BUSINESS)
China Afrika China-Afrika-Kooperationsforum Hu JintaoPicha: Reuters

Mkopo huo ni mara mbili zaidi ya kiasi ambacho China iliahidi kwa kipindi cha miaka mitatu katika mwaka wa 2009 na ndio wa karibuni zaidi katika msururu wa misaada na mikopo inayotoa kwa nchi nyingi za bara Afrika zinazokumbwa na umaskini.

Ahadi hiyo inaonekana kuimarisha uhusiano mzuri wa China na bara la Afrika, ambalo ni muuzaji wa mafuta na mali ghafi kama vile shaba na uranium kwa nchi hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu ulimwenguni na ya pili kwa ukubwa kiuchumi.

Lakini mikopo hiyo huenda isiwe habari njema kwa nchi za magharibi ambazo zinaishutumu China kwa kupuuza uiukaji wa haki za binaadamu katika ushirikiano wake wa kibiashara na Afrika, hasa katika tamaa ya China ya kuulisha uchumi wenye njaa ya raslimali na ambao unaozidi kukua.

China ina miradi mingi ya ujenzi wa miundo mbinu barani Afrika
China ina miradi mingi ya ujenzi wa miundo mbinu barani AfrikaPicha: AP

Hu alipuuzia hofu kama hiyo katika hotuba yake kwa wananchi katika Ukumbi wa Great Hall, mkutano uliohudhuriwa na viongozi akiwemo rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma na mwenzake wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang Nguema, mtu anayeshutumiwa vikali na makundi ya haki za binaadamu kama mmoja wa viongozi wafisadi zaidi ulimwenguni.

China kusaidia katika maendeleo

Rais wa China alisema nchi hiyo kwa moyo mkunjufu na dhati inaunga mkono nchi za Kiafrika kuchagua mkondo wao zenyewe wa maendeleo, na itazisaidia kuimarisha uwezo wao wa maendeleo. Aliongeza kuwa mikopo hiyo mpya itasaidia katika sekta za miundo mbinu, kilimo, utengenezaji bidhaa na maendeleo ya biashara ndogo ndogo na ya kadri barani Afrika.

Umoja wa Ulaya – EU umekataa kile inachokiita kuwa ni mbinu ya “kitabu cha hundi cha China” ya kufanya biashara na bara Afrika, ukisema utaendelea kuitaka nchi hiyo kuonyesha uongozi mzuri na matumizi ya wazi ya fedha kutoka kwa washirika wake wa kibiashara.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ameuambia mkutano huo kuwa uzoefu wa zamani wa kiuchumi kati ya Afrika na Ulaya unaweka haja ya kuwa maini wakati wa kusaini mikataba ya ushirikiano na nchi nyingine.Alisema bara la Afrika lina furaha kuwa katika uhusiano wake na China mambo yote yamekuwa ya usawa na kwamba mikataba iliyofikiwa ni ya manufaa kwa pande zote husika. Aliongeza kuwa Afrika bila shaka ina uhakika kwamba nia ya China ni tofauti na ile ya bara la Ulaya, ambayo hadi sasa inaendelea kuashiria linataka kuzishawishi nchi za Afrika kwa manufaa yao pekee.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ameikaribisha hatua ya China
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ameikaribisha hatua ya ChinaPicha: picture-alliance/dpa

Urafiki wa China na Afrika unarejea katika miaka ya hamsini, wakati nchi hiyo ilipounga mkono mavuguvugu ya ukombozi barani humo wakati wa vita vya kuziangusha utawala wa kikoloni wa nchi za Magharibi.

Mashirika ya Kichina yanayomilikiwa na serikali barani Afrika pia yanakabiliwa na shutuma za kuwaleta wafanyakazi wan chi hiyo kujenga miradi inayofadhiliwa na serikali kama vile barabara na hospitali, wakati ikipeleka mali asili na kuzitengenezea nchini China, na kuacha kidogo katika nchi hizo za Afrika

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef