1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Ujerumani zakaribiana zaidi katika biashara

Sekione Kitojo
24 Mei 2018

Ujerumani  na  China  zimeahidi  kuunga  mkono  makubaliano  ya kinyuklia  na  Iran  na  kutoa  wito  kwa  mazungumzo  na  Korea kaskazini kuendelea  wakati wa ziara  ya  kansela Angela  Merkel nchini  China leo.

https://p.dw.com/p/2yGwM
China Peking - Angela Merkel bei treffen mit Xi Jinping
Picha: picture alliance/AP Photo/J. Lee

Mbali  na  kukubaliana  katika  baadhi  ya  mengi  ya  masuala muhimu  ya  usalama  duniani, Merkel  na  viongozi  hao wa  China wameahidi  kuimarisha  ushirikiano  katika  masuala  kama  biashara na  teknolojia. Rais Xi Jinping  amesema  ushirikiano  kati  ya  China na  Ujerumani  ni  mapana  na  ya  kina  kuliko  wakati  wowote mwingine, hapo  kabla."

China Peking - Angela Merkel bei treffen mit Xi Jinping
Angela Merkel katika mazungumzo na viongozi wa ChinaPicha: picture-alliance/AP Images/J. Lee

Merkel  pia alitoa  wito  wa  kuimarisha  mahusiano , akisema kwamba  nchi  hizo  mbili "haziwezi kukaa  na  kubweteka  hivi  sasa , licha  ya  kila  kitu  ambacho  kimepatikana." amesisitiza  umuhimu wa  kuyafikia  masoko  na  ushirikiano  na  mataifa  mengine. Katika mkutano wa  hapo  kabla  na  waandishi  habari , pamoja  na  waziri mkuu  wa  China  Li  Keqiang , Merkel  alisema  makubaliano  na Iran sio mazuri  sana, lakini mbadala una shaka  zaidi.

Hali  ya  baadaye  ya  makubaliano  na  Iran ,  yenye  lengo  la kupunguza  kasi ya  hatua  za  Iran  kuelekea  kupata  silaha  za kinyuklia, yameingia  mashakani  baada  ya  Marekani  mapema mwezi  huu  kuamua  kujitoa  kutoka  katika  makubaliano  hayo yaliyotiwa  saini  na  mataifa  yenye  nguvu  duniani  na  kurejesha vikwazo  dhidi  ya  nchi  hiyo.

Makampuni ya  Ulaya  kukimbia  Iran

Vikwazo  huenda  vikayafukuza  makampuni  ya  Ulaya  kutofanya biashara  nchini  Iran , hali  itakayoacha  nafasi  kwa   mataifa mengine  kuingia, Merkel  alisema , akidokeza  kuhusu  uwezo  wa China  kujihusisha  zaidi  na  Iran.

China Peking - Angela Merkel bei treffen mit Xi Jinping
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kushoto)akisalimia na rais wa China Xi Jinping(kulia)Picha: picture alliance/dpa/M. Kappeler

"Kufuta  makubaliano  hayo  kunahatarisha  amani  na  uthabiti katika eneo  hilo," Li  amsema. Viongozi  hao  wawili pia  wametoa  wito kwa  rais  wa  Marekani  Donald Trump  na  kiongozi  wa  Korea kaskazini Kim Jong Un  kuendelea  na  majadiliano  kwa  ajili  ya kuondoa   kabisa  silaha  za  kinyuklia  katika   Korea kaskazini.

Trump  na  wawakilishi  kutoka  Korea  kaskazini  wamesema wanaweza  kuvunja  mazungumzo  hayo  ya  kihistoria  kati  ya Marekani  na  Korea  kaskazini, yanayopangwa  kufanyika  mwezi Juni.

Merkel  alisema  ameona "mambo  yenye  kuleta  matumaini  sana hivi  karibuni" kuhusiana  na   uondoaji  wa  silaha  za  kinyuklia katika  rasi  ya  Korea.

Kuhusiana  na  biashara, Li  aliyaahidi  makampuni  ya  Ujerumani kwamba  sekta  ya  fedha  na  huduma  nchini  China  itafungua milango  zaidi.

Usawa  wa masoko

"Hatutaacha  kufungua  milango," alisema   katika  mkutano  na wafanyabiashara  wa  Ujerumani  na  China. Merkel  alitoa  wito  wa kuweza  kuingia  kwa  usawa  katika  masoko  ya  nchi  hizo  mbili  na mfumo wa  ushirikiano  ukiwa  na  viwango  sawa "

"Tunaweza  kuona  kwamba  katika  sekta  ya  magari, ushirikiano kati ya  Ujerumani  na  China  ni  wa  karibu  sana, kuna  mengi yanafanyika  na  ndio sababu  tunataka kufanyakazi  kupata mkataba wa  maelewano MOU ambao  utajumuisha  maendeleo  ya  teknolojia mpya , kama magari yanayokwenda  bila  dereva."

China | Bundeskanzlerin Merkel mit chinesischem Ministerpräsidenten Li Keqiang
Waziri mkuu wa China Li Keqiang(kushoto) akizungumza na kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kulia)Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

"Suala  la  kupata  fursa  ya  kuingia  katika  soko  na  kufanya  hivyo kwa  upande  mwingine  litachukua  jukumu  kubwa " katika mahusiano  kati  ya  China  na  Ujerumani , Merkel  alisema.

Biashara  kati  ya  China  na  Ujerumani  imefikia  euro  bilioni  190 mwaka  jana. Lakini  wachunguzi  wanasema  biashara  kati  ya mataifa  hayo na  hali  ya  wasi  wasi  imekuwa  ikiongezeka  katika miezi  ya  hivi  karibuni.

Mwandishi:   Sekione  Kitojo / dpae

Mhariri: Yusuf, Saumu