1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China inaionya Taiwan dhidi ya kujitafutia uhuru

Mwakideu, Alex4 Machi 2008

Mda mfupi baada ya kuongeza bajeti yake ya kijeshi, China imeshutumu jaribio la Taiwan la kupata uhuru kamili ikidai inahatarisha usalama wake

https://p.dw.com/p/DHxx
Wanajeshi wa China wakisimama wima kulinda bunge la nchi hiyoPicha: AP

Mda mfupi baada ya China kuongeza bajeti yake ya maswala ya kijeshi kwa takriban asilimia 18, Rais wa nchi hiyo Hu Jintao ameshutumu juhudi za Taiwan za kujitafutia uhuru kamili akidai zinatishia usalama China.


Matamko ya Hu yanakuja wiki moja kabla ya uchaguzi wa Urais wa Taiwan ambayo pia inapanga kujiunga na Umoja wa Mataifa kama nchi binafsi. Zaidi anasimulia Alex Mwakideu...


Rais wa China Hu Jintao ametoa mwito  wa mazungumzo kati ya nchi hiyo na Taiwan.


Vile vile amewaambia wanasiasa wanaopigania uhuru wa nchi hiyo kwamba China itawakaribisha iwapo watageuza kauli yao.


China imesisitiza kuiongoza Taiwan tangu pande hizo mbili zilipogawanyika mwaka wa 1949 kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Sasa inakitaka kisiwa cha Taiwan kikubali kuungana nayo hata kama ni kwa kutumia nguvu.


Nchi hiyo imekuwa na wasi wasi haswa kuhusu uchaguzi wa Urais wa Taiwan ambao utafanyika machi tarehe 22 sawa na uteuzi wa wanachama wa Umoja wa Mataifa ambao huenda ukaikubali Taiwan kama mwanachama wake na kupelekea uhuru kamili wa nchi hiyo.


Hata hivyo China ambayo imedai kwamba uhuru wa Taiwan unatishia usalama wake imeongeza bajeti ya jeshi la nchi hiyo kwa asilimia 17.6 mwaka huu na kusisitiza kwamba ongezeko hilo ni la kiasi licha ya shutuma za Marekani.


Msemaji wa bunge la China ameambia wanahabari kwamba nchi hiyo itatumia dola bilioni 57.2 kwa maswala ya kijeshi mwaka huu wa 2008.


Akitangaza hesabu hiyo Jiang Enzhu aliionya Taiwan kwamba mipango yake wa kutegea kuteuliwa kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa mnamo tarehe 22 mwezi huu unaleta hali ya wasi wasi miongoni mwa pande hizo mbili.


Kadhalika Jiang amesema ongezeko la bajeti hiyo ya kijeshi linakuja baada ya ongezeko lengine la mwaka jana ambalo halikutosheleza mahitaji ya kijeshi nchini humo na kwamba fedha za mwaka huu zitatumika kwa mishahara ya wanajeshi na pia kuongeza uwezo wa kiteknologia katika jeshi.


Jiang amesema China imekuwa ikiongeza bajeti yake katika miaka ya hivi majuzi kutokana na uchumi wa nchi hiyo unaokuwa kwa haraka na njia za serikali za kujitafutia fedha.


Ameongezea kwamba bajeti ya jeshi la China mwaka jana ilikuwa asilimia 1.4 ikilinganishwa na ya Marekani ambayo ilikuwa asilimia 4.6 na ya Uingereza ambayo ilikuwa asilimia 3.


Kuwekwa wazi kwa bajeti ya China kumekuja baada ya Marekani kutoa ripoti inayoonyesha wasi wasi juu ya kuongezeka kwa matumizi ya fedha kwa jeshi la nchi hiyo.


Marekani imesema bajeti ya China ya Mwaka jana ilikuwa kati ya dola bilioni 97 na dola bilioni 139 tofauti na China inayosema kwamba bajeti yake ilikuwa ya dola bilioni 45.


Marekani pia imezua hofu kuhusu utengenezaji wa meli na silaha za kisasa, pamoja na jaribio kwa silaha ya kukabili satelite lililofanywa mwaka jana na China. Nchi hiyo pia imeilaumu China kwa kudai inajaribu kutafuta njia za kuchunguza tarakilishi zake za kijeshi.


Hata hivyo wizara ya nchi za nje ya China imepinga vikali ripoti hiyo ikisema haina ukweli ndani yake.


Japan kwa upande wake imeiunga mkono Marekani ikisema kwamba jamii ya kimataifa inaendelea kuwa na wasi wasi kwasababu China haiweki wazi maswala yake ya kijeshi.


Marekani inadai nguvu zaidi za kijeshi zimeendelea kuegemea upande wa China iwapo Taiwan ipo dhabiti.


Akiyajibu hayo msemaji wa wizara ya mambo ya nchi ya nje huko China Qin ameiambia Marekani iwache kuizia Taiwan silaha na imalize uhusiano wake wa kijeshi na kisiwa hicho.


Msemaji wa bunge la China nae Jiang ameionya Taiwan akisema kwamba itapata hasara kubwa iwapo uteuzi wake wa kuingia katika Umoja wa Mataifa utakubaliwa na umma.


Bunge la China The National People's Congress litapasisha rasmi bajeti ya mwaka huu katika vikao vyake vitavyoanza kesho na kuendelea hadi Machi 18.