1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chimbuko na tisho la virusi

Kriesch, Adrian5 Desemba 2014

Virusi vya Ebola viligunduliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka wa 1976 na watafiti wa magonjwa katika kijiji kimoja kwenye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (zamani ikiitwa Zaire)

https://p.dw.com/p/1Dzeu
Ebola Virus
Picha: AP

Virusi vya Ebola ni vidogo mno kuweza kuonekana kwa macho. Huonekana kama uzi kupitia kwa darubini. Virusi hivi viligunduliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka wa 1976 na watafiti wa magonjwa katika kijiji kimoja kwenye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (zamani ikiitwa Zaire). Virusi hivi vilipewa jina la Ebola kuashiria jina la mto unaopakana na kijiji hicho, ambao ni Mto Ebola. Baadaye kukazuka miripuko mingine mitatu nchini humo na vilevile nchini Sudan katika miaka ya ‘70, lakini kisha virusi hivyo vikapotea hadi mwaka wa 1994 wakati ugonjwa huo ulipozuka tena. Kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola nchini Gabon, ndio ulikuwa mwanzo wa kusambaa kwa virusi hivi hadi katika mataifa mengine ya Afrika Magharibi.

Ebola Virus Aufnahme mit Elektronenmikroskop
Picha: Reuters/NIAID

Ugonjwa huu wa Ebola umezuka mara 20 sasa, ingawa mara nyingi umekuwa ukidhibitiwa. Na wakati wote huo ugonjwa huu ulipozuka, idadi ya watu walioambukizwa haikuwa kuzidi 430. Kitisho cha sasa cha Ebola nchini Guinea kilizuka mwaka 2013 na kisha kwa haraka virusi vikasamba hadi nchini Sierra Leone na Liberia ambako kufikia sasa umewaua watu zaidi ya 6,000 na wengine zaidi ya 10,000 kuambukizwa virusi hivyo. Ugonjwa huu sasa umetangazwa kuwa janga katika mataifa hayo.

Mojawapo ya sababu zinazotajwa kuchangia kusambaa kwa virusi vya ugonjwa huu wa Ebola, ni kwamba mwanzoni mataifa yaliyoathirika na hata jamii ya kimataifa ilipuuza uzito wa janga hili.

Ugonjwa wa Ebola ni kana kwamba ulikuwa “unaogelea katika bahari ya taifa lisilojali, kujidanganya, na lisilo na uwezo na ufahamu wa kupambana na kusambaa kwa ugonjwa huu," anasema mtaalamu wa masuala ya virusi nchini Nigeria, Oyewale Tomori.

Kuna maswali mengi kuliko majibu. Mfano, nini kinachotokea mwilini baada ya mtu kuambukizwa Ebola? Je, vijana wananafasi nzuri ya kupambana na Ebola kuliko wazee? Miakia 40 kabla ya kuzuka kwa mripuko wa sasa, ni watu 2,500 pekee waliofariki kutokana na Ugonjwa wa Ebola, idadi ambayo ni ndogo sana ukilinganisha na watu wanaoambukizwa virusi vya ugonjwa wa Ukimwi au kifua kikuu kila siku. Jamii ya kimataifa bado haijafaulu kupata njia bora za kupambana na ugonjwa huu wa Ebola.

Tangu kuzuka kwa ugonjwa huo katika mataifa ya Afrika Magharibi, juhudi za kupata dawa ya kuutibu zimeimarishwa kote duniani. Shirika la Afya Duniani (WHO) lina matumaini ya kutoa chanjo kwa maelfu ya watu wanaoishi katika mataifa yanayoathirika zaidi na ugonjwa huu kufikia katikati mwa mwaka 2015. Na kufikia mwishoni mwa mwaka huo wa 2015 shirika hilo linatarajia litakuwa limetoa chanjo kwa watu milioni moja dhidi ya ugonjwa huo.