1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chavez azikwa

8 Machi 2013

Aliyekuwa rais wa Venezuela, Hugo Chavez, anazikwa leo huku viongozi wa mataifa mbalimbali wakihudhuria mazishi hayo kumuaga kiongozi aliyeenziwa mno katika Amerika ya Kusini.

https://p.dw.com/p/17tUy
Venezuela's Vice President Nicolas Maduro (L), Brazil's former President Luiz Inacio Lula da Silva (2nd L), Brazil's President Dilma Rousseff (C) and Rosa Virginia, daughter of Venezuela's late President Hugo Chavez, view Chavez's coffin during a wake at the military academy in Caracas March 7, 2013, in this picture provided by the Miraflores Palace. Chavez will be embalmed and put on display "for eternity" at a military museum after a state funeral and an extended period of lying in state, acting President Nicolas Maduro said on Thursday. REUTERS/Miraflores Palace/Handout (VENEZUELA - Tags: POLITICS OBITUARY) ATTENTION EDITORS - THIS IMAGE WAS PROVIDED BY A THIRD PARTY. FOR EDITORIAL USE ONLY. NOT FOR SALE FOR MARKETING OR ADVERTISING CAMPAIGNS. THIS PICTURE IS DISTRIBUTED EXACTLY AS RECEIVED BY REUTERS, AS A SERVICE TO CLIENTS
Venezuela Hugo Chavez CaracasPicha: Reuters

Marais na viongozi 55 wa nchi kadhaa wanatarajiwa kuhudhuria mazishi ya Chavez wakiwemo rais wa Cuba Raul Castro, rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad,rais wa Brazil Dilma Rousseff na wa Belaruss Alexander Lukashenko miongoni mwa wengine wengi.

Mrithi wake kisiasa makamu wa rais wa taifa hilo Nicolas Maduro ameahidi kuuhifadhi mwili wa Chavez ambaye sera zake za kisosholisti ziliwapendeza mno masikini na kuwaudhi matajiri wa taifa la Venezuela ili usioze kama ulivyofanyiwa mwili wa aliyekuwa kiongozi wa mrengo wa kushoto Lenin na kuwekwa kwenye jeneza la glasi ili uonekane milele.

Maduro kuapishwa leo

Spika wa bunge nchini humo Diosdado Cabello amesema baada ya mazishi hayo ya kitaifa ya Chavez hii leo, Maduro anatarajiwa kuapishwa rasmi kama rais wa muda wa taifa hilo kabla ya kuitishwa uchaguzi. Baraza la kitaifa la uchaguzi lina jukumu la kuweka tarehe ya uchaguzi wa urais ambao sharti uitishwe katika kipindi cha siku thelathini zijazo kuambatana na katiba.

Rais wa muda wa Venezuela Nicolas Maduro
Rais wa muda wa Venezuela Nicolas MaduroPicha: Reuters

Mwili wa Chavez baadaye utapelekwa katika kambi ijulikanyo kama Mountain Barracks ambayo kwa sasa imebadilishwa kuwa jumba la makumbusho ya harakati za ukombozi wa taifa hilo. Ni katika kambi hiyo ya kijeshi ambapo Chavez alianzisha jaribio lilotibuka la kuipindua serikali ya Carlos Anres Perez mnamo tarehe 4 mwezi Februari mwaka 1992. Kukamatwa kwake baada ya kutibuka kwa jaribio hilo ndiko kulikomfanya shujaa na kumpa ushindi katika uchaguzi wa mwaka 1998.

Huku hali ya kisiasa ikionekana kuwa tete kutokana na kifo cha Chavez,Maduro ametangaza kuwa muda wa umma kuuona mwili wa kiongozi huo umeongezwa kwa siku nyingine saba baada ya sherehe za mazishi yake leo. Serikali imesema zaidi ya watu milioni mbili kutoka kila pembe ya taifa hilo wamekuja kuutizama mwili wake tangu Jumatano.

Wasiwasi baada ya Chavez

Chavez ambaye aliugua saratani kwa karibu miaka miwili amefariki akiwa na umri wa miaka 58 na wengi wa raia wa taifa hilo wameingiwa na wasiwasi kuhusu kama mrithi wake ataweza kulidhibiti taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta na kuendeleza sera zake zilizoonekana kuwapa afueni watu wa kiwango kidogo cha mapato na mataifa jirani hasa Cuba.

Vijana wakiomboleza kifo cha Chavez.
Vijana wakiomboleza kifo cha Chavez.Picha: Reuters

Maduro aliye na umri wa miaka 50 anatarajiwa kumenyana katika kinyang'anyiro cha urais na kiongozi wa upinzani nchini humo Henrique Capriles aliyeshindwa na Chavez mwezi Oktoba mwaka jana.

Mwandishi: Caro Robi/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf