1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto za Yemen

P.Martin2 Juni 2008

Uasi kaskazini mwa nchi; hali ya kutoridha upande wa kusini; kampeni ya al-Qaeda iliyoibuka upya pamoja na wimbi la wakimbizi wa Kiafrika ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili nchini masikini Yemen.

https://p.dw.com/p/EBVb
Yemen's President Ali Abdullah Saleh, candidate of the ruling Peoples' General Congress waves to his supporters in his last election campaign in the capital Sana'a Monday, Sept. 18, 2006. On Wednesday, 9.2 million Yemenis, including 3.9 million women, go to the polls to choose a new president for a seven-year term and members for local councils. (AP Photo/Mohammed Al-Quadi)
Rais wa Yemen Ali Abdullah Saleh akiwapungia wafuasi wake kwenye kampeni ya uchaguzi uliopita Septemba,2006.Picha: AP

Hali ya matatizo inayozidi kuwa mbaya nchini Yemen, imesababisha wasi wasi hata nje ya nchi hiyo.Tangu miaka minne iliyopita,serikali ya Yemen inapambana na uasi wa kundi la Zaydi la madhehebu ya Kishia, linaloongozwa na Abdul-Malik al-Houthi,huku Sanaa ikisema kuwa kundi hilo linasaidiwa kifedha na Iran. Mapambano hayo kwenye Wilaya ya Saada iliyo kaskazini mwa nchi,yameua mamia ya watu na maelfu wengine wamepoteza makaazi yao.Mwezi uliopita mapigano hayo yalizidi kuwa mabaya baada ya shambulizi la bomu msikitini kusababisha vifo vya watu 15.

Mwezi Aprili,kusini mwa nchi maandamano ya kudai ajira yaligeuka kuwa machafuiko ya siku 10 na eneo hilo lenye mafuta na ambako wengi wanahisi kuwa hawafaidiki,lilitoa wito wa kujitenga.Yemen inajaribu kupanua uchumi wake, wakati uzalishaji wa mafuta ukipunguka nchini humo.Lakini mashambulizi ya wanamgambo wa al-Qaeda yaliyoua watalii 10 mwaka jana,yameathiri mradi uliotaka kuimarisha utalii nchini humo.

Ingawa mashambulizi makubwa kama yale yaliyofanywa dhidi ya manowari ya Marekani mwaka 2000 na ile ya Ufaransa hapo 2002 hayakutokea tena,Yemen imeshuhudia mashambulizi zaidi dhidi ya watalii,balozi na majengo ya serikali.Machi iliyopita makombora yaliyolenga ubalozi wa Marekani yaliangukia shule iliyo jirani na kuwajeruhi wasichana 13.Ubalozi wa Uitalia nao ulinusurika chupu chupu na shambulizi kama hilo mwezi Aprili.Kundi la Al-Qaeda lilidai kuwa ndio lililohusika na mashambulizi yote mawili.Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha kupiga vita ugaidi kilicho katika Shule ya Kijeshi ya West Point nchini Marekani, kundi la al-Qaeda nchini Yemen limedhihirisha kuwa lina uwezo wa kuibuka upya kwa nguvu.

Bei ya chakula ikizidi kupanda katika masoko ya kimataifa,hali ya mvutano na kutoridhika inaongezeka katika nchi iliyo miongoni mwa mataifa masikini kabisa duniani.Yemen inaagizia kutoka nje sehemu kubwa ya chakula chake.Ardhi nyingi hutumiwa kwa kilimo cha Qat mmea maarufu unaolewesha.Yemen imepatiwa mabilioni ya Dola na wafadhili wa kimataifa kwa ahadi kuwa itafanya mageuzi na kukomesha ulajirushwa. Lakini wananchi ambao wengi wao huishi sehemu za ndani,hawakunufaika hivyo.

Kusini mwa nchi,hasira za umma dhidi ya eneo la kaskazini linalotuhumiwa kupora mali,ni hali inayohatarisha mafanikio makuu ya Rais Ali Abdullah Saleh-yaani makubaliano ya mwaka 1990 yaliyoziunganisha Yemen ya kaskazini na ya kusini iliyokuwa na sera za kikomunisti.Rais Saleh aliechaguliwa tena mwaka 2006 amekumbana na changamoto mbali mbali na kukomesha jeribio la eneo hilo la kusini kutaka kujitenga.

Mwezi uliopita katika jitahada ya kupunguza udhibiti wa mamlaka,serikali ilianzisha uchaguzi wa mabaraza ya mitaa kuchagua magavana wa wilayani,ambayo hapo awali walikuwa wakiteuliwa na serikali kuu.Lakini makundi ya upinzani yalisusia uchaguzi huo kwa madai kuwa hawakuwakilishwa kihaki katika mabaraza hayo. Wachambuzi wa kisiasa wanasema,uchaguzi huo umeonyesha kuwa serikali kuu ingali ikidhibiti mamlaka lakini hasira za umma pia zinazidi kuongezeka.