1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Champions League:Schalke yasonga mbele, Bremen nje!!

25 Novemba 2010

Schalke 04 ikicheza nyumbani imecharuka na kuichabanga Olympic Lyon mabao 3-0 na kufuzu kwa raundi ya mtoano katika ligi ya mabingwa barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/QHgf
Wachezaji wa Schalke wakishangilia ushindiPicha: AP

Hata hivyo pamoja na kufungwa huko, Lyon pia imefuzu kwa hatua hiyo.Mabao ya Schalke yaliwekwa wavuni na Jefferson Farfan na Klaas-Jan Huntelaar.

Wakati Schalke ikifuzu kwa hatua hiyo, timu nyingine ya Ujerumani Werder Bremen imetupwa nje ya michuano hiyo baada ya kufungwa mabao matatu kwa bila na timu ya Tottenham Hotspur ya Uingereza.

Flash-Galerie Fussball Champions League Tottenham Hotspur Werder Bremen
Mshambuliaji wa Tottenham Younes Kaboul(wa 5 kushoto) akipachika bao huku mlinda mlango wa Werder Bremen Tim Wiese akiduwaa.Picha: AP

Katika mechi nyingine hiyo jana mabingwa watetezi Inter Milan walipata ushindi wa taabu mbele ya Twente Enschede kwa kuifunga bao 1-0, huku Hapoel Haifa ya Israel ikitamba nyumbani kwa kuikandika Benfica ya Ureno mabao 3-0.

Valencia iliunguruma vilivyo katika uwanja wake wa nyumbani kwa kuisambaratisha Bursaspor kwa mabao 6-1, il hali bao la Wayne Rooney kwa mkwaju wa penalti dakika tatu kabla ya mpira kumalizika, lilipa ushindi Manchester United wa bao 1-0 dhidi ya Rangers.

Ama Panathinaikos ilishindwa kutamba nyumbani pale ilipochapwa mabao 3-0 na Barcelona, lakini Rubin Kazan walitumia vyema uwanja wao wa nyumbani kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya FC Copenhagen

Mwandishi:Aboubakary Liongo

Mhariri:Sekione Kitojo