1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama tawala Ukraine chadai kushinda

29 Oktoba 2012

Chama tawala cha Ukraine leo kimedai kushinda katika uchaguzi wa bunge uliofanyika jana, huku matokeo ya awali yakionyesha kinakabiliwa na ushindani kutoka kwa vyama pinzani vya Vitaly Klitschko na Yulia Tymoshenko.

https://p.dw.com/p/16YhB
Kura zikihesabiwa na Tume ya Uchaguzi ya Ukraine
Kura zikihesabiwa na Tume ya Uchaguzi ya UkrainePicha: picture-alliance/dpa

Waziri Mkuu wa Ukraine Mykola Azarov ameelezea uhakika wake kwamba chama tawala kitashinda viti vingi katika bunge jipya baada ya uchaguzi wa jana, ambao mataifa ya Magahribi yanaona ni mtihani mkubwa kwa demokrasia ya Ukraine kutokana na kufungwa kwa mpinzani wa Rais Victor Yanukovich.

Rais wa Ukraine Victor Yanukovich
Rais wa Ukraine Victor YanukovichPicha: DPA

Hata hivyo chama cha bingwa wa masumbwi Vitaly Klitschko kinaonekana kupoteza matarajio yake huku chama cha mchezaji soka Andriy Shevchenko kikikuwa kinaonekana kushindwa vibaya katika uchaguzi huo.

Chama cha Rais Yanukovich kimepata asilimia 35.6 ya kura dhidi ya asilimia 21.5 ilizopata chama cha upinzani cha Tymoshenko. Katika taarifa yake, tume ya uchaguzi imezingatia asilimia 40 ya kura zilizopigwa kwa mfumo sawa wa kuamua viti nusu vya bunge jipya. Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa chama hicho tawala pia kilitarajiwa kushinda angalau viti 110 kati ya 225 vya bunge. Akielezea kuhusu uchaguzi huo Azarov amesema wanategemea kuwa chama tawala kitapata viti vingi katika bunge jipya. Aidha, chama cha kikomunisti kilikuwa kimeshika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 15.1ya kura na chama kipya cha UDAR kilichojitenga na Klitschko kikiwa kimepata asilimia 12.8.

Urusi na Umoja wa Ulaya wanaufatilia uchaguzi huo

Uchaguzi huo wa jana ni mkubwa wa kwanza kufanyika nchini Ukraine ambao umeonyesha mvutano kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi tangu kiongozi aliyefanya mapinduzi ya chungwa mwaka 2004, Tymoshenko kushindwa katika uchaguzi wa urais mwanzoni mwa mwaka 2010, uchaguzi uliomuweka madarakani Yanukovich. Urusi inaufatilia uchaguzi huo kwa makini, huku Umoja wa Ulaya ukitaka viwango vya demokrasia vizingatiwe, wakati ambao Ukraine inaendelea kusisitiza nia yake ya kujiunga na umoja huo. Waangalizi wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya-OSCE wanatarajia kutoa maamuzi yao kuhusu uchaguzi huo baadae hii leo, ambayo yanafatiliwa kwa karibu kabisa kuona iwapo kuna udanganyifu uliofanywa.

Tymoshenko mwenye umri wa miaka 51, alikamatwa Agosti mwaka uliopita wa 2011 na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kupatikana na hatia ya  kutumia vibaya madaraka, hukumu ambayo mataifa ya Magharibi na wafuasi wake wanaona kama ni njama za kisiasa zinazofanywa Yanukovich. Wasiwasi kuhusu utawala wa miaka miwili wa Yanukovich ulioigawa Ukraine kutoka kwenye mkondo wake wa demokrasia uliosababisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton na Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton kutoa wito wa kufanyika uchaguzi utakaozingatia demokrasia.

Viongozi wa Urusi na Umoja wa Ulaya
Viongozi wa Urusi na Umoja wa UlayaPicha: dapd

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP,RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman