1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama tawala cha Afrika kusini, ANC, kukutana haraka

Oumilkheir Hamidou
11 Februari 2018

Shinikizo linazidi kumtaka rais Jacob Zuma ang'atuke madarakani. Kamati ya maamuzi ya chama tawala African National Congress-ANC inakutana kwa kikao cha dharura kesho jumatatu.

https://p.dw.com/p/2sTUk
Südafrika, Protest gegen den Präsidenten Jacob Zuma
Picha: picture-alliance/T.Hadebe

 

Wanachama wa ngazi za juu wa chama tawala ANC watakutana kwa kikao cha dharura kesho katika wakati ambapo rais Jacob Zuma anazidi kutiwa kishindo ajiuzulu.

Baraza tendaji la taifa, taasisi muhimu ya maamuzi nchini humo, itakutana mjini Pretoria, taarifa imesema. Mazungumzo katika ngazi ya juuu ya chama cha ANC yamekuwa yakiendelea tangu jumapili iliyopita, katika wakati ambapo Waafrika Kusini wanasubiri kwa hamu kubwa tangazo la kung'atuka rais Zuma.

Jacob Zuma anatiwa kishindo ajiuzulu kabla ya muhula wake kumalizika kutokana na kashfa za kuhusika na rushwa.

Wakati huo huo makamo wa  rais Cyril Ramaphosa alionekana katika kanisa kuu la St.George mjini Cape Town, kuadhimisha siku aliyoachiwa huru rais wa zamani, marehemu Nelson Mandela. Nelson Mandela aliachiwa huru kutoka jela ya Victor Verster, February 11 mwaka 1990. Mwaka huu inaadhimishwa pia miaka mia moja tangu alipozaliwa rais huyo wa kwanza mweusi tangu ulipomalizika mfumo wa ubaguzi wa rangi na mtengano nchini Afrika Kusini-Apartheid.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma na makamo wakeCyril Ramaphosa (Kutoka kushoto)
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma na makamo wakeCyril Ramaphosa (Kutoka kushoto)Picha: Reuters/S. Sibeko

Ramaphosa anapewa nafasi nzuri ya kumrithi Zuma kama rais wa Afrika Kusini

Akiwa mwenyekiti wa ANC, Ramaphosa ndie anaeongoza sherehe za kuzaliwa Nelson Mandela. Mwanaharakati huyo wa haki za wafanyakazi aliyegeuka mfanyabiashara, amechaguliwa Desemba mwaka jana kukiongoza chama tawala, baada ya muhula wa pili wa Zuma kama mwenyekiti wa chama hicho kumalizika.

Pindi Zuma akijiuzulu kama rais wa Afrika Kusini, Ramaphosa anapewa nafasi nzuri ya kumrithi. Vyombo vya habari vya Afrika Kusini vinaripoti kwamba Zuma anajadiliana na wanachama wa ngazi ya juu wa ANC kuhusu vigezo vya kung'atuka .

Katika taarifa iliyochapishwa kupitia mtandao wa Instagram na mke mmojawapo wa Jacob Zuma, bibi Thobeka Madiba-Zuma anaashiria rais Zuma hatong'atuka bila ya mapambano. Lakini familia ya Zuma iliomba radhi baadae kutokana na taarifa hiyo.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa

Mhariri: Jacob Safari