1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Labour chamtimua mhafidhina John Howard

25 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CSqX

Enzi mpya imeanza hii leo nchini Australia,baada ya kiongozi wa chama cha Labour Kevin Rudd kumshinda Waziri Mkuu John Howard katika uchaguzi wa siku ya Jumamosi.Kevin Rudd katika hotuba yake ya ushindi alisema,wakati umewadia kuandika ukurasa mpya katika historia ya Australia.Akaongezea kuwa Australia imetazama mustakabali wake.Waaustralia wameamua kusonga mbele kama taifa;kujiandaa kwa mustakabali wao na kuungana kuandika ukurasa mpya katika historia ya taifa lao.

Mhafidhina Howard,mshirika mkuu wa Rais wa Marekani George W.Bush,alitawala kwa takriban miaka 12 na alifanikiwa kunyanyua uchumi wa Australia,lakini alipoteza umaarufu wake miongoni mwa wapiga kura wengi,hasa kuhusika na msimamo wake katika vita vya Irak na mabadiliko ya hali ya hewa duniani.Kevin Rudd ameahidi kufuata sera mpya kuhusu mada hizo mbili.