1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Kijani kuongoza serikali Baden-Württemberg

12 Mei 2011

Nchini Ujerumani, kwa mara ya kwanza kabisa, amechaguliwa waziri mkuu wa serikali ya jimbo kutoka chama cha walinzi wa mazingira "Die Grüne".

https://p.dw.com/p/RNYG
New state governor of the German federal state Baden-Wuerttemberg Winfried Kretschmann of the Green Party speaks the oath during the swearing in ceremony at the parliament of Stuttgart, Germany, Thursday, May 12, 2011. Kretschmann is the first Green state governor in Germany in a center-left coalition with the Social Democrats. (Foto:Michael Probst/AP/dapd)
Waziri Mkuu mpya wa jimbo la Baden-Württemberg, Winfried KretschmannPicha: dapd

Winfried Kretschmann wa chama cha Kijani "Die Grüne", hii leo ameteuliwa rasmi na wabunge katika jimbo tajiri la kusini-magharibi ya Ujerumani, Baden-Württemberg. Chama hicho kilijinyakulia asilimia 24 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa jimbo uliofanyika Machi 27. Kwa hivyo, chama cha Kijani, kimeweza kuunda serikali katika jimbo hilo, pamoja na chama cha kisoshalisti SPD, kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Ujerumani. Hiyo ni hatua muhimu kabisa katika historia ya chama cha Kijani. Kwa mara ya kwanza kabisa tangu kuundwa kwake katika miaka ya 1970s, chama hicho kinaongoza serikali ya jimbo. Na sio jimbo lo lote bali ni katika jimbo la kihafidhina la Baden-Württemberg ambako chama cha CDU kilikuwa kikiongoza kwa miongo kadhaa. Lakini kufuatia uchaguzi wa Machi 27, chama cha Kijani kimezidi kuwa maarufu kama anavyoeleza mkuu wa masuala ya kisiasa wa chama hicho Steffi Lemke:

" Bila shaka sera za chama cha Kijani zinazidi kuvutia na zinaungwa mkono.Katika kipindi cha mwezi wa Machi na wa Aprili idadi ya watu waliojiandikisha uanachama,imeongezeka sana. Hata mada zinazohusika na mazingira zinapewa umuhimu zaidi."

Baada ya mwalimu wa zamani Winfried Kretschmann kuungwa mkono na wabunge 73 kutoka 138, chama cha Kijani kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Ujerumani imeshika wadhifa wa Waziri Mkuu katika serikali ya jimbo. Chama cha Kijani, kimewahi kushiriki katika serikali za majimbo mengi na kuanzia mwaka 1998 hadi 2005 ilishika madaraka pamoja na chama cha SPD katika serikali kuu mjini Berlin. Lakini daima chama hicho kilikuwa mshirika mdogo na kila mara kilipaswa kupigania malengo yake.

Lakini katika jimbo la Baden Württemberg, chama cha Kijani kwa mara ya kwanza kabisa kinashika usukani. Safari hii SPD ni mshirika mdogo na hakina budi kuizoea hali hiyo mpya. Kwa kiwango fulani, CDU bado ni chama chenye nguvu katika jimbo la Baden-Württemberg, lakini baada ya kupata pigo kubwa katika uchaguzi uliopita, sasa kinapaswa kukaa upande wa upinzani kwa mara ya kwanza, baada ya kutawala kwa 58 iliyopita. Chama cha Kijani ambacho daima kimekuwa na msingi imara katika jimbo la Baden-Württemberg, sasa kinapaswa kuzoea jinsi ya kuongoza madaraka.

Mwandishi: Werkhäuser,Nina/ZPR

Mhariri: Yusuf Saumu