1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bush atetea Ubepari kabla ya mkutano wa G20

Kalyango Siraj14 Novemba 2008

Viongozi wa mataifa 20 duniani ya G20 wanakutana Marekani kupanga mkakati wa pamoja utakaosaidia kushughulikia mgogoro wa kifedha unasambaa.

https://p.dw.com/p/Fum8
Rais Bush, kushoto na Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia, kushoto.Picha: AP Photo

Mwenyeji wa mkutano huu Marekani ambayo hapo awali ilikuwa inasitasita,sasa inataka mpango tekelezi ambao utaupiga msasa mfumo mzima wa kimataifa kuhusu fedha, upatikane baada ya kikao cha mkutano huo.

Rais George W.Bush akizungumza alhamisi kuhusu uchumi akiwa mjini New York amesema kuwa viongozi watakao hudhuria mkutano huo wanakubaliana kuhusu mkakati mmoja ambao ni kujadili mgogoro wa kifedha unaoendelea na pia kuweka msingi wa mageuzi ambayo,alifafanua kuwa yatasaidia kuzuia matatizo kama hayo yasitokee wakati ujao.

Mkutano huo unatarajiwa kuja na mbinu madhubuti za kuzuia mgogoro huu wa kifedha kutobadili sura na badala yake kukaufanya uchumu kudorora kwa mda mrefu.

Lakini yeye David Resler, mwanauchumi mkuu wa kampuni ya amana za Nomura Securities ya mjini New York Marekani ana maoni taofauti.Anasema kuwa hatarajii kuwa mkutano huo utakuwa na jambo la maana.

Mgogoro huu wa kifedha ulianza mwaka mmoja uliopita wakati soko la nyumba la nchini Marekani lilipopata matatizo. Matatizo hayo yalisamba kama moto hadi katika sekta ya fedha na pia kuikumba sekta nzima ya mikopo ya nyumba.

Hata hivyo ahadi pamoja na hatua zinazoahidiwa hazitausaidia utawala wa rais Bush kwani muhula wake wa miaka minane unamalizika januari mwakani.Mrithi wake Barack Obama wa chama cha democratic anapasha moto misuli yake kuchukua nafasi yake januari 10.

Miongoni mwa mengine Marekani pia inataka kuona kama mashirika mengine kama vile Benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa IMF yote yanafanyiwa marekebisho ili yaweze kutoa mwanya wa usemi zaidi uchumi unaonukia.

Mkutano ujao unatarajiwa kupatanisha makundi ya mataifa ya G 8 ambayo yana viwanda vingi duniani pamoja na mataifa ya G 20 ambayo ni mataifa yenye uchumi imara na yale yenye uchumi unaozidi kuinukia.

Raia wengi wa Ulaya hasa hasa faransa wanamini kuwa mkutano huu wa G20 utakuwa kama chanzo cha mageuzi lakini sio kupelekea mkutano mwingine kama ule wa Bretton Woods wa pili wa mwaka wa 1944 ambao mkataba wake ulipelekea kuundwa kwa mifumo ya sasa ya kifedha.

Mkutano wa kilele wa mataifa ya G 20 pia unatarajiwa kujadili juhudi za pamoja za kuufufua uchumi wa dunia baada ya China kutangaza mpango wake kuupiga jeki mfumo wake wa uchumi ambao utagharimu dola za kimarekani billioni 586.

Kundi la mataifa 20 liliundwa mwaka wa 1990 na linahusika na uzalishaji wa 85% ya uchumi wa dunia na pia idadi yake ya watu ni takriban theluthi mbili ya watu wote duniani.

Bara la Afrika linawakilishwa katika kundi hilo na Afrika Kusini.Miongoni mwa mataifa mengine wanachama ni Saudi Arabia, Uturuki, Korea Kusini pamoja na Indonesia.