1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yatoa waranti wa kumkamata Buyoya

Daniel Gakuba
1 Desemba 2018

Burundi imetoa waranti wa kimataifa wa kumkamata rais wake wa zamani Pierre Buyoya na maafisa wengine 16, kuhusiana na mauaji ya Melchior Ndadaye, rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.

https://p.dw.com/p/39FUl
Burundi Pierre Nkurunziza, Präsident
Rais wa Burundi, Pierre NkurunzizaPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Mugiraneza

Mwendesha mashitaka mkuu wa Burundi Sylvestre Nyandwi amesema uchunguzi umebainisha kuwa watu hao walihusika katika kupanga na kutekeleza mauaji dhidi ya Ndadaye, rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, wa kwanza pia kutoka jamii ya Wahutu. Mauaji hayo yalifuatiwa na machafuko makubwa ya kikabila, ambamo watu zaidi ya 300,000 waliuawa.

Buyoya kwa wakati huu ni mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Mali, na ni mtu anayeheshimiwa barani Afrika na katika jumuiya ya kimataifa. Buyoya, Mtutsi aliyeingia madarakani kupituia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1987 alikubali kushindwa na Ndadaye katika uchaguzi wa mwaka 1993.

Lakini Ndadaye alihudumu madarakani kwa miezi minne tu, akauawa na kundi la wanajeshi Watutsi wenye misimamo mikali, katika jaribio la mapinduzi lililoitumbukiza Burundi katika mzozo ambao athari zake zinaendelea hadi leo.

Katika waranti wake, Burundi inazitaka nchi wanakoishi washutumiwa hao kuwakamata na kuwarejesha nchini kwao, ikisema ni muhimu watu hao kuhojiwa kuhusu mchango wao katika mauaji ya Ndadaye.

Miongoni mwa 16 wanaotuhumiwa pamoja na Buyoya, 11 walikuwa maafisa wa kijeshi, na 5 waliobakia walikuwa raia wenye mahusiano ya karibu na Buyoya.

Serikali ya sasa ya Burundi inaongozwa na chama cha Cndd-FDD cha Rais Pierre Nkurunziza, kikiwa tawi la kundi la zamani la waasi wa kihutu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga