1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burundi yatakiwa kukomesha mauaji yanayofanywa na polisi dhidi ya raia.

30 Aprili 2008

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human rights Watch, limeitaka Burundi isitisha vitendo vya kinyama ambavyo vimekuwa vikifanywa na Kikosi maalumu cha Polisi wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/DrOT
Mwenyekiti wa AU, Rais Jakaya Kikwete kulia akiwa na rais George W.Bush wa Marekani kushoto.Picha: AP

Hii ni kwa mujibu wa taarifa yake iliyotolewa leo kuhusu masuala ya haki za binadamu.

Ripoti hiyo imekuja wakati Rais wa Nchi hiyo Pierre Nkurunziza akitarajiwa kukutana na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Jakaya Mrisho Kikwete.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo na Human Rights Watch,mwaka jana kikosi maalumu cha polisi wa burundi kiliwazuia na kuwatesa raia.

Katika ripoti yao ya kurasa arobaini na mbili waliyoiita "kila siku asubuhi wananipiga" mwaka 2007, vitendo vya kinyama ambavyo vimekuwa vikifanywa na kikosi maalumu cha polisi kifupi-GMIR,vinafikia ishirini na moja kwa vile vya kupiga raia na kuwatesa.

Baadhi ya waathirika wa vitendo hivyo wamekuwa wakitoa taarifa kwa shirika hilo la kutetea haki za binaadamu wakielezea jinsi walivyokuwa wakikamatwa kiholela pasipo sababu, wakipigwa kwa marungu na fimbo na wengine kuuawa.

Vitendo vingine ni kulazimishwa kutoa hongo na vitu ili wawezee kuachiwa huru.

Kikosi cha GMIR kilitumwa kwenda katika mji wa Rutegama katika jimbo la Muramvya lililoko Mashariki mwa muji wa bujumbura kupambana na uhalifu unaoongezeka na kuzuia kundi la waasi nchini humo-FNL, kuwaingiza wapiganaji wapya katika kundi hilo.

Hata hivyo maofisa wa Serikali wamekataa kulizungumzia suala hilo.

Human Rights Watch imesema vikosi vya polisi vya nchi hiyo ya Afrika ya kati ni mchanganyiko wa vikosi vya waasi wa zamani, wanajeshi na wanamgambo ambao walipata mafunzo kamili.

Shirika hilo limeitaka Serikali ya nchi hiyo ambayo ni miongoni mwa nchi masikini duniani na inayotegemea zaidi misaada kutoka sehemu mbalimbali duniani,kurekebissha sheria zake za makosa ya jinai na kuziweka katika viwango vya Kimataifa.

Wito huo wa Human Rights Watch umetolewa wakati rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza alitarajiwa kukutana na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Uganda Yoweri Museveni kwa lengo la kujadili machafuko katika nchi hiyo mzalishaji mkuwa wa kahawa.

Ni kiwango kidogo sana cha mambo yaliyokwisha kushughulikiwa kwa miaka kumi na nne iliyopita ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyokadiriwa kuuwa watu laki tatu na kuporomosha Uchumi wa nchi hiyo.

Mapigano ya hivi karibuni yalikuwa ni baina ya Majeshi ya Serikali na Waasi wa kundi la FNL yaliyozusha hofu nyingine kuwa huenda yakaibua awamu nyingine ya umwagaji damu nvhini humo.

Aidha taarrifa iliyotolewa na jeshi la nchi hiyo imesema kuwa mapigano ya hivi karibuni yaliyotokea pembezoni mwa muji wa Bujumbura yamesababisha vifo vya watu hamsini na moja.