1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ujerumani larefusha jukumu la ATALANTA

18 Desemba 2009

ATALANTA-Vita dhidi ya maharamia Pembe ya Afrika.

https://p.dw.com/p/L73n
Bundestag-Bunge la Ujerumani.Picha: AP

Kwa wingi mkubwa wa kura, Bunge la Ujerumani-Bundestag, liliidhinisha jana huko Berlin, kurefusha jukumu la ule ujumbe wa ATLANTA unaoongozwa na Umoja wa Ulaya la kupambana na uharamia katika Pembe ya Afrika.Ni kura 74 kati ya 577 za wabunge waliohudhuria kikao hicho ndio tu waliopinga. Ujerumani, inachangia kwa manuwari na wanajeshi wake 240 katika kikosi hicho.

Wanajeshi 240 wa Ujerumani waliomo ndani ya manuwari iitwayo "Bremen" watapitisha siku kuu za Krismasi mwaka huu katika bahari ya Hindi.Wao ni sehemu ya kikosi cha Umoja wa Ulaya kilichoitwa "ATALANTA" kinachopiga doria katika pwani ya Pembe ya Afrika.Mwaka baada ya kuanza mradi huu, waziri wa nje wa Ujerumani Guido Westerwelle,alielezea jana Bungeni mafanikio yake: anaeleza kwamba, hujuma nyingi za maharamia katika meli za biashara ziliweza kuzuwiliwa .Isitoshe, meli zote zilizopakia shehena za Mpango wa chakula wa Umoja wa mataifa ,ziliweza kuwasilisha shehena zao hadi Somalia salama usalimini.

Westerwelle aliliambia Bunge:

"Huu ni mradi wa kutulinda sisi,kulinda meli zetu,njia zetu za misafara ya biashara na kuwalinda wasomali ili nao shehena za misaada ya kiutu ziwafikie."

Shehena hizo za misaada ndio uti wa maisha ya wasomali milioni 3-asema Thomas Kossendey,katibu wa dola wa wizara ya ulinzi:

"Vikosi vya mradi wa "ATALANTA" tangu ulipoanza mradi huu, vimezima zaidi ya hujuma 120 za maharamia.Zaidi ya maharamia 70 waliweza kupelekwa Kenya kwa mashtaka.Naamini,idadi ya hujuma zilizofanikiwa,zilizopungua, ni ushahidi pia kwamba, tumefanya kazi nzuri huko."

Lakini mtu asitarajie miujiza kutoka manuwari 30,alisema mwanasiasa huyu kutoka chama-tawala cha CDU.Eneo la ulinzi na kupiga doria katika pwani ya Pembe ya Afrika ni kubwa mno na hivyo huwezi kulilinda lote .Hivi sasa maharamia nao wanafanya ujambazi wao mbali kabisa na pwani ya Somalia.Kwa maoni ya chama cha mrengo wa shoto cha Ujerumani-LINKE , huo ni ushahidi kwamba, mradi huo wa kupiga doria hauna maana yoyote.

Mwandishi: Werkhäuser,Nina/ZR/ Ramadhan Ali

Mhariri:Abdul-Rahman