1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Congress kupiga kura leo

Josephat Charo23 Machi 2007

Viongozi wa chama cha Democratic nchini Marekani wameapa kuendelea kushinikiza wanajeshi wa Marekani walio nchini Irak waondoke ifikapo mwaka ujao huku mswada wa kuongeza fedha kwa vita nchini Afhanistan na Irak ukipigiwa kura bungeni hii leo. Sambamba na hayo balozi wa Marekani nchini Irak anayeondoka, Zalmay Khalilizad, ameahidi kuendelea kusaidia juhudi za kuleta amani nchini Irak.

https://p.dw.com/p/CHHd
Nancy Pelosi wa chama cha Democratic
Nancy Pelosi wa chama cha DemocraticPicha: AP

Wabunge wa chama cha Democtrats katika baraza la wawakilishi wameandaa mswada unaotaka wanajeshi wa Marekani waondoke Irak kufikia tarehe 31 mwezi Agosti mwaka ujao huku jopo la baraza la senate likiidhinisha mswada unaotaka wanajeshi hao waondoke kufikia mwezi Machi.

Wabunge wa chama cha Democtrats wanaamini wana idadi ya kura zinazohitajika kuupitisha mswada huo. Baadhi ya Wademocrats waliokuwa wakipinga mswada huo wamebadili msimamo wao baada ya siku kadhaa za mabishano ndani ya chama kuhusu swala hilo. Bunge la Congress linajianda kuupigia kura hii leo mpango wa kuongeza bajeti ya vita nchini Irak na Afghanistan kwa kiwango cha dola bilioni 124 za kimarekani.

Mbunge wa chama cha Democtratic, David Obey, mwenyekiti wa kamati ya bunge na muasisi wa mswada huo, amesema watajaribu kuilekeza Marekani katika njia mpya. Naye kiongozi wa chama cha Democtratic, Steny Hoyer, akasema hatua hiyo itasaidia kumaliza sera mbaya ya Marekani nchini Irak.

Miswada yote miwili inatakiwa kuainishwa kabla kusainiwa na rais George W Bush ili iwe sheria. Rais Bush amesema bunge la Congress linatakiwa kuupitisha mswada huo haraka iwezekanavyo bila kutumia fedha nyingi wala kuweka masharti. Ikulu ya White house mjini Washington imeonya kwamba mpango wa chama cha Democrats utakabiliwa na kura ya turufu ya rais na hauna nafasi ya kufanyika sheria.

Sambamba na taarifa hizo balozi wa Marekani nchini Irak anayeondoka Zalmay Khalilzad alisema jana anajuta kwamba anaondoka nchini humo lakini akalitaja eneo la Wakurdi kama mfano mzuri wa utulivu nchini Irak. Kiongozi huyo mzaliwa wa Afghanistan aliyetimiza umri wa miaka 56 hapo jana, aliahidi kuendelea kuzisaidia juhudi za kutafuta amani nchini Irak iwapo ataidhinishwa kuwa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo Khalilzad alisema litakuwa jukumu la viongozi wa Irak kukubaliana na kuiunganisha nchi hiyo. Zalmay Khalilzad aliyasema hayo alipofanya ziara ya kuliaga eneo la Wakurdi kaskazini mwa Irak wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya pili ya mwaka mpya wa Kikurdi wa Nowruz.

Na huko nchini Irak jeshi la Marekani limetangaza mwanajeshi wake mmoja aliuwawa jana wakati bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara liliporipuka karibu na kituo cha upekuzi magharibi mwa mji mkuu Baghdad. Kifo cha mwanajeshi huyo kimeiongeza idadi ya wanajeshi wa Marekani waliouwawa tangu uvamizi wa Irak kufikia 3,226.