1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge kumua kuhusu operesheni ya kijeshi

P.Martin17 Oktoba 2007

Bunge la Uturuki hii leo linakutana mjini Ankara kuamua ikiwa liidhinishe operesheni ya kupeleka vikosi vyake ndani ya ardhi ya Irak kushambulia vituo vya waasi wa Kikurd.

https://p.dw.com/p/C77j
Waziri Mkuu wa Uturuki,Recep Tayyip Erdogan akihotubia bunge mjini Ankara
Waziri Mkuu wa Uturuki,Recep Tayyip Erdogan akihotubia bunge mjini AnkaraPicha: AP

Ikiwa bunge la Uturuki litatoa idhini yake,kama inavyotarajiwa,basi Waziri Mkuu Recep Tayyip Erdogan atakuwa na muda wa mwaka mmoja kutayarisha operesheni ya kijeshi dhidi ya waasi wa Kikurd wa chama cha PKK,kaskazini mwa Irak. Chama hicho kinalaumiwa kuhusika na mashambulizi ya hivi karibuni ndani ya Uturuki,katika mgogoro wa zaidi ya miongo miwili.

Uturuki inazituhumu Marekani na Irak kuwa hazijitahidi vya kutosha kuwadhibiti kiasi ya wanamgambo 3,000 wa Kikurd wanaojificha katika eneo la mpakani,kaskazini mwa Irak.Ankara inasema,chama cha PKK kinachohesabika kama ni kundi la kigaidi nchini Uturuki na nchi nyingi zingine,kina uhuru mkubwa kaskazini mwa Irak na kinastahmiliwa na utawala wa Kikurd katika eneo hilo.Vile vile Ankara inasema,waasi wa PKK katika eneo hilo linalodhibitiwa na Wakurd wa Kiiraki, hupata silaha za kuishambulia Uturuki mpakani. Majuma mawili yaliyopita,waasi wa Kikurd kutoka ardhi ya Irak walishambulia vituo vya Uturuki.Kwa mujibu wa serikali ya Uturuki,mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya wanajeshi na raia darzeni kadhaa na sasa Erdogan anataka kuchukua hatua ya kijeshi kukomesha mashambulizi ya aina hiyo.

Lakini Marekani,kwa mara nyingine tena imeionya Uturuki kutochukua hatua ya kijeshi.Hata serikali ya Irak ina wasi wasi kuwa uamuzi huo wa Uturuki utavuruga utulivu uliokuwepo kaskazini mwa Irak.Kwa hivyo,siku ya Jumanne ilipeleka ujumbe wake mjini Ankara kuzungumza na viongozi wa Uturuki.

Naibu-Rais wa Irak,Tareq al-Hashemi alipokutana na waziri mkuu wa Uturuki alisema,anaielewa hasira ya Uturuki inayosababishwa na vitendo vya PKK kutoka kaskazini mwa Irak.Akaongezea kuwa Baghdad imedhamiria kukomesha mashambulizi ya mpakani yanayofanywa na waasi wa Kikurd.Wakati huo huo al-Hashemi ameiomba serikali ya Uturuki iwape viongozi wa Irak muda,ili waweze kushirikiana na Uturuki kutenzua tatizo la waasi wa PKK.

Kwa mujibu wa gazeti la Sabah,al-Hashemi amekwenda Iraq na ujumbe uliotoka kwa Rais wa Irak,Jalal Talabani ambae ni Mkurdi na Massoud Barzani alie kiongozi wa utawala wa ndani wa Wakurd kaskazini mwa Irak.Viongozi hao wamesema, wapo tayari kujadiliana na Ankara tatizo la PKK.