1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Buhari aagiza uchunguzi ripoti ya HRW

1 Novemba 2016

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ameshtushwa na ripoti iliyotolewa jumatatu hii (31.10.2016) na shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch, inayohusu unyanyasaji wa kingono katika makambi ya wakimbizi nchini humo.

https://p.dw.com/p/2Ryg3
Deutschland Berlin - Der Nigerianische Präsident Muhammadu Buhari
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Masaa machache baada ya shirika hilo kutoa ripoti hiyo, Rais Buhari pamoja na kueleza mshituko alioupata ametaka kufanyika kwa uchunguzi juu ya suala hilo. Ripoti ya Human Rights Watch inaeleza kuwa maafisa wa serikali, vikosi vya usalama na maafisa wengine waliwabaka na kuwatumikisha kingono kiasi ya wanawake na wasichana 46 waliokuwa wakiishi kwenye kambi ya Maiduguri, iliyoko Kaskazini Mashariki wa mwa Jimbo la Borno.

"Madai haya yamechukuliwa kwa uzito mkubwa", amesema msemaji wa rais wa nchi hiyo.

Kulingana na ripoti hiyo, wahanga wanne waliofanyiwa mahojiano mwezi Julai walikiri kupatiwa dawa za kulewesha na kubakwa, wakati wengine 37 wakisema walilazimishwa kushiriki ngono kupitia ahadi za kufunga ndoa ama misaada ya kifedha. 

"Ni aibu na ukatili mkubwa kwamba watu ambao walitarajiwa kuwalinda wanawake hawa na wasichana ndio wanawafanyia mashambulizi na kuwanyanyasa, amesema mtafiti kutoka shirika hilo la haki za binaadamu, Mausi Segun.  

Aidha utafiti wa maoni uliofanywa na shirika jingine la utafiti nchini Nigeria, NOI umeonyesha kwamba asilimia 66 ya raia 400 walioyakimbia makazi yao kutoka eneo la kasikazini Mashariki mwa nchi hiyo wanatajwa kuhusishwa na vitendo kama hivyo vya unyanyasaji wa kingono. 

Flüchtlingslager DIkwa Nigeria
Baadhi ya wakimbizi wanawake wanaoishi kwenye moja ya kambi zilizoko Jimbo la Borno.Picha: picture-alliance/dpa/next24online

Aidha ripoti nyingine iliyotolewa mwezi mei mwaka huu na shirika la misaada lililopo Borno, nayo ilivitaja vitendo vya ubakaji na vingine vya unyanyasaji wa kingono kama masuala muhimu ya kuangaziwa katika makambi yote 13 na baadhi ya jamii zinazowahifadhi raia hao wanaotafuta makazi kutoka eneo lote la Maiduguri. 

Katika hatua nyingine, nchini Nigeria, Gavana wa Jimbo hilo la Borno, ambalo ndilo hasa linakabiliwa na kitisho cha Boko Haram, Kashim Shettima, ameyatuhumu baadhi ya mashirika ya Umoja na mataifa na mengine yanayotoa misaada kwa matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya misaada ya wakimbizi. Ameyatoa madai hayo mbele ya Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa mataifa linalojihusisha na idadi ya watu, UNFPA, ijumaa iliyopita.

Gavana huyo amedai kwamba Umoja wa mataifa umetumia Dola Milioni 50 kununulia magari yenye uwezo wa kuzuia risasi kupenya. hata hivyo, msemaji wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya binaadamu nchini Nigeria Orla Fagan amesema magari hayo yaliytolewa na wahisani, na si kwamba walitumia fedha za wakimbizi.

Hata hivyo Gavana Shettima hakuzungumzia madai yaliagizwa na seneti kufanyiwa uchunguzi kwamba taasisi za serikali ya nchi hiyo zilikuwa zikiiba chakula cha misaada kilichopelekwa Maiduguri, kwa ajili ya wakimbizi, na badala yake gavana huyo alizungumzia zaidi ya wafanakazi 500 wa umoja wa Mataifa kuvamia Maiduguri, huku uwepo na matumizi yao vikizua maswali mengi. 

Kulingana na Umoja wa Mataifa, inakadiriwa watu Milioni 2.7 katika ukanda huo wamekimbia makazi yao kutokana na kitisho cha kundi la wapiganaji la Boko Haram nchini Nigeria, Chad, Cameroon na Niger.

Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Yusuf Saumu