1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS:Viongozi wa Ulaya wakutana na Jumuiya ya Milki za Kiarabu

15 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC1y

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wamefanya mkutano ambao haukutarajiwa na Viongozi wa Jumuiya ya Milki za Kiarabu mjini Brussels,Ubelgiji.Mkutano huo unalenga kuunga mkono juhudi za kufufua mpango wa amani wa Mataifa ya Kiarabu katika eneo la Mashariki ya kati.

Kwa mujibu wa Waziri wa mambo ya kigeni ya Ujerumani Frank Walter Steinmeier aliyezungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo,fursa iliyojitokeza inapaswa kuungwa mkono ili kufikia malengo ya kupata amani katika Mashariki ya Kati.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Milki za Kiarabu Amyr Moussa kwa upande wake anasisistiza kuwa wako tayari kuafikiana na Israel ila wanapaswa kushirikiana.Kundi la washirika wane wakuu wa kimataifa wanaohusika na mpango wa amani wa Mashariki ya Kati ambao ni Umoja wa Ulaya,Marekani,Urusi na Umoja wa Mataifa wana jukumu la kutimiza lengo la kufikia amani katika kipindi cha muda uliowekwa.

Mpango huo ulioanzishwa na Saudia mwaka 2002 na kufufuliwa tena katika mkutano wa Jumuiya hiyo mwezi machi mjini Riyadh unalenga kurejesha uhusiano na Israel ila baada ya kurejesha ardhi iliyonyakuwa kutoka mataifa ya Kiarabu mwaka 67 vilevile kuundwa kwa taifa la Palestina na kurejeshwa kwa wakimbizi wake.

Umoja wa Ulaya ulivunja uhusiano wake na serikali ya Palestina baada ya Chama cha Hamas kuingia madarakani mwaka jana.Bwana Amyr Moussa na Waziri wa mambo ya nje wa Saudia Saud al Faisal anatoa wito kwa Umoja wa Ulaya kushirikiana moja kwa moja na serikali ya Palestina vilevile kuanzisha tena msaada wa pesa uliositishwa tangu Hamas kuingia madarakani.