1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS:Sarkozy aahidi kuondoa nakisi ya bajeti ya Ufaransa kufikia 2010

10 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBkL

Rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy amesema atajaribu kuondoa nakisi ya bajeti ya nchi yake ifikiapo mwaka 2010.Hata hivyo rais huyo wa Ufaransa baada ya kukutana na mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels ameonya mbele ya waandishi wa habari kwamba licha yakuwa lengo lake ni kutimiza ahadi hiyo mwaka 2010 mageuzi aliyoyapanga ili kuimarisha kwa kasi uchumi wa Ufaransa huenda asiweze kuyatimiza kabla ya mwaka 2012.

Aidha rais Sarkozy amesema hajamaanisha kwamba sheria za bajeti ya Umoja wa ulaya zilegezwe hasa kwa ajili ya Ufaransa.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Peer Steinbrück ambaye hakufurahishwa na hotuba ya rais wa Ufaransa amesema hiyo haitasaidia kuhakikisha uimara wa Umoja huo na ukuaji wa uchumi wake.

Wakati huo huo mawaziri wa fedha wa Umoja huo wanatazamiwa kukutana leo hii kujadili juu ya kuchagua mtu atakayechukua nafasi ya mkurugenzi mkuu wa shirika la fedha duniani IMF baada ya mkurugenzi wa sasa wa shirika hilo Rodrigo Rato kusema anataka kujizulu ifikiapo mwezi wa Oktoba.