1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS:EU yaitaka Marekani kuzungumza na Iran

28 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC6L

Mkuu wa siasa za Nje katika Umoja wa Ulaya, Javier Solana, ameiomba Marekani, kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na Iran juu ya mpango wa nchi hiyo wa nuklia.

Solana amesema kuwa baada ya siku mbili za mazungumzo na Ali Lariana ambaye ni afisa wa Iran katika mzozo huo wa nuklia mjini Ankara Uturuki, amebaini kuwa Iran iko tayari kwa mazungumzo hayo.

Amesema kuwa ana uhakika, Lariani na kiongozi wa kiroho wa Iran Ali Khamenei wako tayari kuupokea mkono wa mazungumzo utakaonyooshwa na Marekani.

Mjini Washington Marekani imesema kuwa msimamo wake ni ule ule kwamba Iran kwanza iache kurutubisha nishati ya nuklia kabla ya kukaa meza moja kuzungumza.

Msemaji wa Usalama wa Taifa wa nchi hiyo, Gordon Johndroe amesema kuwa Marekani imetoa nafasi kwa Iran kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 27, lakini kwa sharti la kuacha kwanza mpango wake huo.

Marekani na nchi nyingine za Magharibi zinaamini kuwa Iran inataka kuunda silaha za nuklia kitu ambacho serikali ya Tehran imekipinga na kusema kuwa kinu chake chake cha nuklia ni kwa matumizi ya kawaida tu.